Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inatoa mkopo kwa asilimia miamoja kwa Wanafunzi wanaofaulu zaidi masomo ya Sayansi kidato cha sita na kusomea nyanja za Sayansi, Elimu Tiba, Uhandisi, Hisabati na TEHAMA Elimu ya Juu
Mkenda amesema hayo Agosti 24, 2024 baada ya kuzindua Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi Dimbani na Dahalia ya Wanafunzi wa kike katika Skuli hiyo Kisiwani Unguja, akiwasisitiza Walimu kuwahimiza Wanafunzi kutumia fursa hiyo kikamilifu.
Waziri huyo ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kwenda sambamba na kasi ile ya uendelezaji wa elimu ambayo ndio mwelekeo wa Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw. Khamis Abdulla Said amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imegharamia kwa asilimia miamoja mradi wa ujenzi wa Skuli ya Sekondari Kizimkazi Dimbani iliyopo Kisiwani Unguja kwa kutumia fedha za direct indicators, ambapo jumla ya Sh. Milioni 223 zimetumika.
Ameeleza hayo wakati akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi huo, unajumuisha madarasa manne, chumba cha maabara na maktaba, ofisi ya Mwalimu Mkuu na Ofisi ya Walimu na kwamba itakuwa na uwezo wa kutoa Wanafunzi 180 kwa wastani wa Wanafunzi 45 kila darasa.