Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi(CRB) Mhandisi Consolata Ngimba akiwa na wajumbe wengine wa bodi hiyo wakimsikiliza Mhandisi wa Ujenzi kutoka kampuni ya ‘China Hobour Engeneering Company’ inayotekeleza ujenzi wa Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, wakati wa ziara ya Bodi hiyo.
*************************************
BODI ya Makandarasi nchini(CRB) inatarajia kuanza kufanya ukaguzi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni za nje ili kubaini kama kuna ushirishikishwaji wa kampuni za wakandarasi za ndani katika miradi hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Bodi hiyo kubaini uwepo wa baadhi ya kampuni zinazotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mikubwa kutoshirikisha kampuni za ndani kama sheria na taratibu zinavyotaka na hivyo kuiathiri sekta hiyo hapa nchini.
Akizungumza wakati wa ziara iliyofanywa na Bodi hiyo kukagua miradi mbalimbali jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi Consolata Ngimba, alisema hatua hiyo imelenga kuwalinda na kuziinua kampuni za kizalendo zilizopo nchini.
Alisema ili kuleta tija katika kampuni hizo hususani kushiriki katika miradi mikubwa ya ujenzi inayofanaywa na kampuni za kigeni, CRB itafanya ukaguzi huo nchi nzima ili kubaini kama kampuni hizo zinatekeleza matakwa ya kisheria ya kuzishirikisha kampuni za wazawa katika miradi hiyo.
“Ukaguzi wetu umebaini kwa kiasi kikubwa kampuni za kigeni zimekuwa hazishirikishi kampuni za hapa ndani na hivyo kuathiri uwezo wa kampuni hizo, hivyo kwa kufanya hivyo tunaamini kuwa kutazisaidia kushiriki katika miradi hiyo” alisema Consolata.
Pia Mwenyekiti huyo wa Bodi ya CRB alizitaka kampuni hizo za kigeni kuhakikisha inatoa nafasi za ushiriki wa miradi mbalimbali inayoitekeleza ili kuepuka kukiuka taratibu za kisheria ambapo kwa kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza matatani ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kufanya kazi katika miradi mingine hapa nchini.
Pia alizitaka kampuni zinazohusika na masuala ya ukandarasi hapa nchini kujenga ushirikiano wa pamoja ili kuwa na nguvu ambazo licha ya kuzisaidia kupata mitaji mikubwa pia itaziwezesha kufanya kazi kwa kipindi kifupi na ufanisi utakaoleta matokeo chanya katika miradi husika.