Waendesha Bodaboda katika picha ya pamoja baada ya semina iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Wilaya ya Kisarawe.
Mmoja wa waendesha Bodaboda akifungua akaunti ya NMB.
Waendesha Bodaboda wakifurahia jambo wakati wakiendelea na mafunzo ya matumizi ya huduma mpya ya MastaBoda.
Mkuu wa Kitengo cha Kadi wa Benki ya NMB- Philbert Casmir, akizungumza wakati akifunga rasmi mafunzo ya matumizi ya huduma mpya ya MastaBoda kwa waendesha Bodaboda wa Wilaya ya Kisarawe na vitongoji vyake. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo na Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB-Vicky Bishubo.
******************************
KAMPENI ya MastaBoda inayoendeshwa na Benki ya NMB kwa ajili ya kuwaunganisha waendesha
Bodaboda katika mfumo wa kibenki wa kupokea malipo kwa Mastercard QR kutoka kwa wateja wa
Benki ya NMB, Benki zilizounganishwa na Mastacard QR pamoja na mitandao ya simu iliyounganishwa
na huduma ya Mastercard QR sasa imevuka boda hadi Kisarawe Mkoani Pwani.
Akizindua kampeni hiyo na kufunga mafunzo ya siku sita yaliyotolewa na NMB kwa waendesha
Bodaboda Wilayani humo, Mkuu wa Wilaya Jokate Mwegelo amesema kampeni hiyo imefika muda
muafaka katika Wilaya yake.
Jokate amesema, kama Wilaya na Serikali wamejipanga kuipokea kampeni hiyo kwa waendesha
bodaboda 150 waliyozitokeza katika mafunzo hayo.
Amesema kupitia kampeni hiyo wanataka vijana wawe mstari wa mbele katika kujenga uchumi wa nchi
na maendeleo ya jamii zao. Pia amewataka vijana kuishi kwa malengo kwani sasa wamepata mfumo
ambao unaipa ulinzi fedha wanayoipata katika kazi zao za kila siku.
Aidha Jokate ameimwagia kongole Benki ya NMB kwa kuipa heshima Kisarawe kuwa sehemu ya pili
kufikiwa na MastaBoda baada ya kuzinduliwa Dar es Salaam miezi miwili iliyopita.
"Nashukuru sana NMB kwa kunipa heshima hii kwa Wilaya yangu ya Kisarawe, naamini hamkupanga
kuanzia hapa baaada ya Dar es Salaam, ila mmeona jitihada zangu asanteni sana. Hakuna mafanikio bila
nidhamu, NMB mmetuletea nidhamu ya pesa pamoja na usalama kwa vijana wetu maana sasa hawatakuwa wanatembea na pesa mfukoni."amesema Jokate.
Nae Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB, Vicky Bishubo amesema NMB imejipanga
kuyafikia makundi mbalimbali ya wajasiriamali ili kuwaongeze thamani katika kukuza uchumi wa nchi.
Amesema MastaBoda ni kampeni ambayo inalengo la kuwafikia waendesha bodaboda zaidi ya Milioni 2
nchi nzima, ila kufikia 2020 watakuwa wamewafikia elfu 75.