Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara Joseph Kibehele akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa warsha hiyo katika chuo cha VETA Mtwara
Mratibu wa mradi huo Francis Komba akisisitiza jambo kwa washiriki wakati akiwasilisha mada juu ya wajibu wa wadau hao katika kufanikisha utoaji mafunzo
Mmoja wa washiriki akichangia mada wakati wa warsha hiyo.
Washiriki wa warsha hiyo ambao ni wadau wa hoteli na utalii wakifuatilia mada wakati wa warsha hiyo.
Washiriki wa warsha wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara baada ya kufungua warsha hiyo.
****************************
NA KITENGO CHA MAWASILIANO VETA TANZANIA
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imekutana na wadau wa sekta ya Hoteli (Ukarimu) na Utalii wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kuweka mikakati ya kuanza kutoa mafunzo kwa ushirikiano kupitia programu ya Uwanagenzi Pacha (Dual Apprenticeship training).
Akifungua warsha hiyo mkoani Mtwara Desemba 17, 2019, Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara Ndugu Joseph Kibehele amesema utoaji mafunzo kupitia programu hiyo unategemea sana wenye viwanda, kampuni na hoteli kushiriki kikamilifu.
“Tunawaomba sana mshiriki katika programu hii ili tuweze kuandaa wafanyakazi wenye viwango mnavyovihitaji kwenye hoteli zenu.”Alisema.
Aliongeza kuwa VETA inatambua umuhimu wa kushirikiana na viwanda katika kutoa mafunzo kwa kuwa ushirikiano huo unawezesha kuandaa nguvu kazi mahiri zaidi inayoendana na mahitaji halisi ya viwanda hasa kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya mafunzo hayo yanafanyika sehemu za kazi.
Mratibu wa programu hiyo Ndugu. Francis Komba alisema kuwa VETA imeamua kutoa mafunzo ya Uanagenzi pacha katika sekta hiyo kupitia mfumo huo baada ya Utafiti wa soko la ajira kufanyika katika mikoa hiyo na kubaini mahitaji makubwa ya wataalamu wa hoteli na utalii kwa ngazi ya ufundi stadi.
Alisema mafunzo katika programu hiyo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye fani ya Ukarimu na Utalii yanatarajiwa kuanza kutolewa mwezi Januari, 2020 kupitia chuo cha VETA Mtwara.
Kwa mujibu wa Komba, mafunzo kupitia programu hiyo yanamwezesha kijana kupata ujuzi wa fani husika akiwa chuoni na sehemu ya kazi, hivyo kumwezesha kwa kiasi kikubwa kujifunza kwa vitendo na kuendana na
mahitaji ya soko la ajira pamoja na kupata uzoefu na uelewa wa mazingira halisi ya kufanyia kazi.
Meneja wa Shangani Apartments Ndugu Athumani Akida amesema kuwa mfumo huo wa mafunzo utasaidia wenye hoteli kupata wafanyakazi bora zaidi kwa kuwa wenye hoteli wanapata fursa ya kushiriki kuwandaa
wakati wa mafunzo. Alisema “Naamini kabisa programu hii itaondoa lile gap linalojitokeza kati ya sisi waajiri na wanafunzi wanaozalishwa vyuoni”.
Naye Afisa Mwandamizi wa hoteli ya BNN Royal Palm Bi. Grace Paul alisema kuwa hoteli yake iko tayari kushiriki kikamilifu katika kutoa mafunzo hayo na kushauri wadau wengine kujitokeza kushiriki kutoa mafunzo kupitia programu hiyo yenye faida kwao.
Mratibu msaidizi wa programu hiyo Ndugu Fahil Challange alisema kuwa hadi kufika mwaka 2023 VETA inatarajia kuzalisha wahitimu 15,000 kupitia programu hiyo kutoka 500 wa sasa na kuongeza fani hadi kufikia tisa kutoka tano zilizoko sasa kutokana na mpango kazi ambao VETA
imeandaa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania ATE.
Mfumo wa utoaji mafunzo ya Uanagenzi pacha unahusisha kuhudhuria mafunzo ya vitendo kwenye karakana na darasani (VETA) na kufanya vitendo zaidi katika sehemu za kazi. Mafunzo hayo ni ya miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka mwanagenzi anatumia wiki 20 VETA na wiki 32 kwa mafunzo ya viwandani.
Mfumo wa mafunzo ya Uanagenzi pacha ulianzishwa mwaka 2011/12 kwa ushirikiano kati ya VETA na Hamburg Chamber of Skills Craft ya Ujerumani ambapo kwa sasa unatekelezwa katika vyuo vinne vya VETA vya Moshi
(Ukarimu na Utalii), Dar es Salaam (Ufundi Umeme na Ufundi Magari), Simanjiro (ufundi ujenzi) na Manyara (Ufundi wa zana za kilimo).