Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Nazareth Mbesa Halmashauri ya wilaya Namtumbo Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa chuo hicho Ezekiel Mapunda(hayupo pichani,wakati wa Jubilei ya miaka 50 tangu chuo hicho kilipoanzishwa mwaka 1974.
Na Mwandishi Wetu,
CHUO cha Ufundi Nazareth Mbesa kinachomilikiwa na Wamisionari wa Kanisa la Bibilia,kimeadhimisha miaka 50 tangu kilipoanzishwa mwaka 1974 na kinatajwa ndiyo chuo cha muda mrefu zaidi katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Chuo hiki kilianzishwa kwa lengo la kuwapatia vijana wa Kitanzania hususani vijana wanatoka katika wilaya ya Tunduru kupata elimu ya ufundi ili waweze kujitegemea katika maisha yao ya baadaye.
Kimsingi chuo hiki ni msaada na mkombozi mkubwa siyo kwa vijana wa Tunduru tu bali wanaotoka mikoa ya Kusini Lindi,Mtwara na Ruvuma kwani tangu kilipoanzishwa mwaka 1974 vijana zaidi 1,100 wamefanikiwa kupata elimu na kozi mbalimbali za ufundi.
Anasema,kwa sasa chuo kina wanafunzi 150 kati yao 110 wanaishi bweni na 40 wanatoka nyumbani na mara kwa mara wanaboresha miundombinu kwa ajili ya mazingira bora ya kujifunzia na kuna vifaa vinavyotolewa kwa wanafunzi wa fani ya useremala na fani nyingine.
Hata hivyo,mwaka 2023 na 2024 Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru iliteua vijana 354 waliomaliza darasa la saba na kidato cha nne ili kujiunga na chuo cha Nazareth,lakini vijana 14 hadi sasa ndiyo waliotumia fursa hiyo kujiunga na chuo na vijana 340 hawakuripoti.
Anafafanua kuwa,vijana 8 kati ya 114 ndiyo waliripoti mwaka 2023 na mwaka 2024 vijana 6 kati ya 240 wameweza kujiunga na chuo hicho,hivyo wengine wameshindwa kutumia vema fursa ya uwepo wa chuo hicho katika wilaya yao kupata ujuzi katika fani mbalimbali.
“hata vijana tulionao katika chuo chetu zaidi ya asilimia 60 wanatoka nje ya wilaya ya Tunduru na asilimia 40 iliyobaki ndiyo wenyeji hata hivyo makuzi yao siyo Tunduru, hapa kuna kazi kubwa ya kuhamasisha wazazi ili waone umuhimu wa kuwaleta vijana wao wapate ujuzi utakaowasaidia kujitegemea katika maisha yao”alisema.
“Chuo chetu kimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla na tunahamasisha wazazi kuleta watoto wao waliomaliza darasa la saba na kidato cha nne ili wapate ujuzi badala ya kukaa nao nyumbani”anasema Mkuu wa chuo Ezekiel Mapunda.
Mapunda anaeleza kuwa,wakati chuo kinaanzishwa kulikuwa na wanafunzi wanane tu wa kiume ambao walipata mafunzo katika fani ya Useremala,na mwaka 1976 iliongeza fani ya magari na mwaka 1994 kilianzisha kozi ya uchongaji na ukelezaji vyuma pamoja na uchomeaji.
Aidha anasema,mwaka 2017 fani mbili mpya za umeme wa majumbani,ushonaji na mapambo zilisajiriwa ili kupanua wigo zaidi kwa watoto wa kike kujiunga na chuo hicho ili waweze kupata ujuzi na na kozi hizo zinatolewa kwa muda wa miaka mitatu.
Mapunda anataja baadhi ya kozi zinazotolewa katika chuo cha Ufundi Nazareth Mbesa ni pamoja na ufundi wa magari,ufundi umeme wa majumbani,ushonaji,Useremala na uundaji na wanapokea wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali.
Anasema,walianza kufanya kazi ya kundisha katika mazingira magumu kwa kutumia chaki kwa kuwa walimu wengi walikuwa Wazungu,hivyo suala la mawasiliano la lugha lilikuwa gumu hasa kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya wilaya ya Tunduru.
“kwa sasa tumepiga hatua kubwa katika ufundishaji kwani tunafundisha kwa kutumia projekta na tumefunga mtandao wa Internet wenye kasi unaotusaidia kupata vifaa vya kufundishia ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi badala ya kufundisha kwa chaki”anasema Mapunda.
Anaeleza kuwa,kwa kawaida uelewa wa mtu unapanuka zaidi anapoona na kusikia,kwa hiyo utaratibu wa uwasilishaji wa mada nyakati hizi ni bora na nzuri sana kuliko mwanzoni kulingana na mazingira ya upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
“uelewa wa mtu unapanuka zaidi anapoona na kusikia,kwa hiyo utaratibu wa uwasilishaji wa mada nyakati hizi ni bora na nzuri sana kuliko mwanzoni kulingana na mazingira ya sasa hivi na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia”alisema Mapunda.
Mapunda anaeleza kuwa,wamejipanga kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mafunzo kwa fani mbalimbali kwa vijana wa Kitanzania ili waweze kunufaika na uwepo wa chuo hicho.
“hakuna gharama anayotozwa mtoto au mzazi,badala yake wazazi wanatakiwa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao hasa wale wanaoishi bweni,Daftari,Bima ya afya,shuka,blanketi,vyombo vya kulia chakula na nguo za kazi.
Katibu Mkuu wa pili wa Shirika la misaada la Kanisa la Bibilia Dunia Klaus Brinkmann anasema,vijana wengi waliosoma katika chuo hicho wamepata kazi kwenye taasisi na idara mbalimbali za Serikali na wengine wakijiajiri,hivyo kuondokana na umaskini na hali ngumu ya maisha na kuzisaidia familia zao.
Anasema,mafanikio haya yametokana na malengo waliyokuwa nayo na kutumia vizuri elimu waliyopata wakiwa chuoni,hivyo anawataka Wanafunzi kutumia ujuzi na elimu wanayoipata kufikiria kujiajiri zaidi badala ya kuajiriwa Serikalini.
Amewaasa kwenda kufanya kazi kwa weledi,kuwa wabunifu,waaminifu na kutengeneza bidhaa bora pindi watakapomaliza mafunzo yao ili kujenga imani kwa wateja kwenye maeneo yao kama wanataka kupata mafanikio.
Mkuu wa tatu wa Misheni Mbesa Karl Warth aliyewakilishwa na Mkuu wa sita wa Misheni hiyo Helga Armbruster anasema,wakati wanaadhimisha miaka 50 ya chuo hicho watu wengi wametoa fedha na michango yao ili kuwawezesha vijana wa Tunduru kupata ujuzi utakao wasaidia katika maisha yao.
Anawataka wazazi na walezi,kuhakikisha wanapeleka watoto kujiunga na chuo hicho na vijana kwenda kupata ujuzi katika fani mbalimbali ambazo zitawasaidia kuondokana na changamoto ya ajira na umaskini.
Karl Warth,amewapongeza wafanyakazi wa chuo kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuimarisha na kuboresha elimu ya ufundi ambayo imewasaidia baadhi ya vijana wa Kitanzania hususani wanatoka wilaya ya Tunduru kujitegemea.
Mmoja wa wahitimu wa chuo hicho mwaka 1993 Selestine Kalo amasema,chuo cha Nazareth kimewapa watu mafanikio na wamekuwa tegemeo kwa familia,jamii na Taifa ikiwemo kuwapa ufundi vijana wenzao wa Kitanzania katika fani mbalimbali.
Hata hivyo,ameshauri uongozi wa chuo kuleta vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia kutokana na kukua kwa teknolojia hasa uwepo wa magari yanayotumia gesi.
Ameiomba jamii,kukiamini na kutumia fursa ya uwepo wa chuo cha Ufundi Misheni Mbesa kupeleka watoto wao kupata ujuzi utakaowasaidia kufanya kazi za kujiletea maendeleo na kujikwamua na umaskini.