Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Dodoma (TAKUKURU),Bw.Eugenius Hazinamwisho, akizungumza wakati akiwasilisha taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi husika.
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Dodoma (TAKUKURU), imeeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu imefanya kazi ya ufuatilaiji wa kuzuia rushwa katika sekta nne na kubaini mapungufu kadhaa katika miradi yake.
Hayo yameelezwa leo Agosti 7,2024 Jijini Dodoma na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Eugenius Hazinamwisho wakati akiwasilisha taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi husika na kuongeza kuwa miradi 12 ya maendeleo ilofuatiliwa yenye thamani ya zaidi ya bilioni 4.
“Katika fuatiliaji huo tulibaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa katika miradi 10 yenye thamani ya Bilioni 3.1, mapungufu hayo ni pamoja na utumiaji wa nondo zilizo chini ya kiwango, matumizi ya mbao hafifu katika utengenezaji wa milango, ujenzi kutoendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika, baadhi ya wazabuni kulipwa kabla hawajamaliza vifaa, wazabuni kulipwa fedha na kuwasilisha vifaa pungufu, matofali na mabati kutofanyiwa ukaguzi wakati wa upokeaji kama kanuni za manunuzi zinavyoelekeza”, amesema.
Naibu huyo ameongeza kuwa mapungufu hayo yamepelekea kufunguliwa kwa majalada ya uchunguzi kwa baadhi ya miradi, huku elimu na ushauri vikitolewa kwa baadhi ya miradi ili wahusika kufanya marekebisho na baadhi ya miradi imeendelea kufanyiwa ufuatiliaji.
Aidha amebainisha vipaumbele vyao kwa kipindi cha mwezi Julai mpaka Septemba vinavyolenga kuzuia vitendo vya rushwa visitokee kuwa ni pamoja na kuongeza kasi ya uelimishaji umma kwa makundi tofauti ya wadau kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi ili wananchi wajue wajibu wao katika kuzuia rushwa.
“Pia tumejipanga kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya rushwa na ufujaji unaoweza kujitokexa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuelimisha umma kwa kutumia njia mbalimbali hasa katika makundi ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa”amebainisha.
Pia ametoa wito kwa wananchi wote kushiriki katika kuzuia vitendo vya rushwa kwani mapambano dhidi ya rushwa ni wajibu wa kikatiba.