………….
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imefanikiwa kukusanya fedha za mapato ya ndani shilingi 51,402,342,226 sawa na asilimia 103 ya lengo la mwaka wa fedha 2023/2024 wakati ikipeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kupokea na kujadili taarifa za utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili-Juni, 2024) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kayombo ambae ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa bajeti ya mapato ya ndani ya mwaka 2023/2024 ilikuwa shilingi 50,097,458,280. Fedha iliyokusanywa ni shilingi 51,402,342,226 sawa na asilimia 103. Alisema kati ya fedha hizo za mapato ya ndani, asilimia 73.4 ilipelekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na asilimia 26.6 ikienda kwenye matumizi mengineyo.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Kayombo alilipongeza Baraza la Madiwani kwa kutenga na kutoa fedha za fidia. “Mheshimiwa mwenyekiti, nilipongeze Baraza la Madiwani kwa kutenga na kutoa fedha. Wananchi 357 wamelipwa fidia ndani ya kipindi cha miezi sita kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kati ya shilingi bilioni 3.4 zilizotengwa. Hatuna upungufu wa kulipa fidia, ni maelekezo ya Chama Cha Mapindzi ngazi ya wilaya na mkoa” alisema Kayombo kwa kujiamini.
Wakati huohuo, aliutaarifu mkutano huo kuwa halmashauri imenunua magari mawili kwa ajili ya kusafisha barabara. Alisema kuwa gari moja lina uwezo wa kufagia barabara kisha mchanga unaofagiliwa ukafyonzwa. Gari la pili linauwezo wa kudeki barabara kwa presha ya maji. Alisema kuwa magari hayo yamenunuliwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Nae Diwani wa Kata ya Tambukareli Juma Michael alitoa rai kwa wananchi kuendelea kulipa kodi na ushuru wa serikali kwa hiari. “Napenda kuwasisitiza wananchi kuendelea kulipa kodi na ushuru wa serikali kwa hiari kwa sababu miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zetu inatokana na kodi. Hivyo, kodi unayolipa ndiyo inayorudi kukuletea maendeleo” alisisitiza Michael.
Ikumbukwe kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilikusanya asilimia 80.6 ya mapato ya ndani