Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL limewataka wakulima nchini kujiunga na vyama vya ushirika ili kunufaika na huduma ya malipo ya mkupuo inayotolewa na shirika hilo kwa wakulima.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la shirika hilo lililopo katika viwanja vya Maonesho vya nanenane Nzuguni Jijini Dodoma Meneja wa biashara mkoa huo Leila Pongwe amesema katika maonesho hayo wamewaletea wakulima huduma hiyo ili kuwasaidia kupokea malipo yao kwa haraka na uhakika.
“Mwaka huu tumewaletea wakulima malipo kwa mkupuo ambayo yanamuwezesha mkulima kupitia vyama vyao vya ushirika yaani mnunuzi analipa kwa mkupuo kwa vyama alafu vyama vinawalipa wakulima kwa kupitia laini zao za T Pesa”,Amesema
Amesema kwa kufanya hivyo kutamsaidia mkulima kupata masoko makubwa na kufanyabiashara kwa uaminifu kwani sasa TTCL inamkongo hadi nje ya nchi hivyo ni rahisi kupata huduma ya T Pesa.
Ameongeza kuwa mpaka sasa wameshaingia mikataba na vyama vya ushirika zaidi ya 100 na vyama hivyo vinapatikana kila mkoa nchini.
Sambamba na hayo amesema katika maonesho hayo pia wametoa huduma ya intaneti ya bure kwa wanaotembelea maonesho hayo.
Aidha kauli mbiu ya huduma hiyo inasema’Lipa malipo ya wakulima kwa mkupuo ukiwa na T PESA’.