******************************
Na Boniphace Richard Dodoma 17/12/2019
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mh: Ummy Mwalimu amewaagiza viongozi wa wilaya na mikoa kufanya mikutano ya hadhara juu ya umuhimu wa kutunza mazingira, kudibiti taka ngumu na ujenzi wa vyoo bora.
Akizungumza kwenye maadhimiso ya wiki ya usafi wa mazingira na mkutano wa maafisa afya wa mikoa, halmashauri na wadau maadhimisho yaliyobebwa na kauli mbiu “Huduma Bora za Afya mazingira na usafi ni kichocheo muhimu cha uchumi endelevu’’.
Aidha amesisitiza kuwa jukumu la wizara ya afya ni kuhakikisha wananchi hawapatwi na maradhi, pia ni wajibu wake kama mbeba dhamana katika kuhakikisha huduma bora za matibabu zinapatikana.
“siwezi kujidai kuwa nafanya kazi vizuri wakati watu wanamaradhi” alisema Ummy
Pia waziri Ummy amewahakikishia maafisa afya wa mikoa, halmashauri na wadau kuwa serikali imedhamiria kuwekeza kwenye kinga pamoja na tiba kwa ujumla. Ambapo amesema kuwa jambo la kwanza linalofanywa na wizara ni kuhakikisha kuwa suala la chanjo kwa wagonjwa linapewa kipaumbele.
“hadi sasa tayari baadhi ya magonjwa yametokomezwa kwa kiasi kikubwa ukiwemo ugonjwa wa ndui” aliongeza Ummy
Awali akitoa salamu kutoka ofisi ya makamu wa Rais, muungano na mazingira naibu waziri wa ofisi bw. Musa Sima amesema ofisi hiyo imepewa jukumu kubwa la kulinda mazingira kwani usafi wa mazingira kwao ni neno pana, huku akiwataka maafisa afya kuwa na ushirikiano lengo likiwa kuhakikisha mazingira yanakuwa katika hali ya ubora.
Kwa upande wake, katibu mkuu wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa baadhi ya mafanikio makubwa ambayo yameletwa na maafisa afya ni pamoja na kusimamia kwa ufanisi mkubwa suala la chanjo na kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa ndui pamoja na polio huku akigusia kampeni ya Taifa ya utekelazaji wa usafi wa mazingira kuwa unaendelea nchini kote.
Sanjari na hayo, mwenyekiti wa Maafisa Afya Mkoa bw. Evance Mkoko amesema kwa upande wa kampeni ya usafi wa mazingira wameweza kuinua kiwango cha mazingira hususani ujenzi wa matumizi ya vyoo bora umefikia asilimia 35.