Na.Alex Sonna-DODOMA
MENEJA wa Shirika la Viwango (TBS) Kanda ya Kati Bw. Nickonia Mwambene, amesema katika maonesho ya Nanenane mwaka huu wanatilia mkazo elimu ya wazalishaji kutumia Viwango katika mnyororo mzima wa uzalishaji kuanzia mashambani, matumizi ya pembejeo bora na uhifadhi wa mazao unaozingatia Viwango.
Mwambene ameyabainisha hayo jana Agosti 5,2024 wakati akizungumza na wandishi wa habari katika banda la TBS katika maonesho hayo yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma ambapo ameongeza kuwa bidhaa salama ni kichocheo cha uchumi wa nchi.
“Kwasababu inakubalika kwa watumiaji, ni rahisi kupata soko la ndani na nje ya nchi, ni rahisi kuvuka katika mipaka ya kiforodha na ni rahisi kushindana sawia katika soko”, amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inawekeza kuwapa elimu ya viwango kwa wazalishaji bure kupitia TBS ili wakidhi ubora na kuwanyanyua ili wakue na kushindana katika soko la bidhaa zinazofanana zilizo katika soko lao.
Pia Serikali kwa kutambua mchango wa wajasiriamali wadogo inatenga kati ya millioni 150-200 kwa mwaka kupitia TBS ili kuwawezesha kupatiwa elimu ya viwango,kufanyiwa ukaguzi wa bidhaa zao na kupatiwa leseni ya kutumia alama ya ubora kwa zile zinazokidhi matakwa ya viwango ili waweze kupeleka bidhaa zao sokoni na kushindana na zile zinazotoka nje ya Nchi.
Mpaka sasa zaidi ya wajisiriamali 1500 wamefaidika na mpango huo.