Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Balozi Amina Salum Ali akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Wizara hiyo Migombani Unguja,kuhusu Tamasha la Sita la Biashara la Zanzibar litaloanza Januari 02 hadi 15 mwaka 2020.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na Wafanyakazi kutoka katika Taasisi mbali mbali wakimsikiliza Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali alipokuwa akitoa Taarifa ya Uzinduzi wa Tamasha la Sita la Biashara Zanzibar litaloanza Januari 02 hadi 05 mwaka 2020 hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara hiyo, Migombani Unguja.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
……………
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar.
Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar imewataka wafanyabiashara , Wenyeviwanda na Taasisi binafsi kushiriki katika tamasha la sita la biashara linalotarajiwa kufanyika January 2 hadi 15 ya mwaka 2020.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari huko ofisini kwake Migombani, Waziri wa Wizara hiyo Balozi Amina Salum Ali amesema lengo la tamasha hilo ni kuwapatia fursa wafanya Biashara kutangaza Biashara zao ndani na Nje nchi.
Amesema wamekuwa wakiandaa Tamasha mara kwa mara kwa madhumuni ya kuwasaidia Wajasiriamali na wananchi watembeaji, kuweza kuona bidhaa kununua pamoja na kupata huduma mbali mbali zitolewazo na Serikali na Taasisi binafsi .
Aidha amesema ni muhimu kwa Wafanyabiashara kushiriki katika tamasha hilo kwani litawapatia nafasi za kutangaza bidhaa kwa kuweza kutambulika ndani na nje ya nchi na kupata soko la uhakika .
” Wafanyabiashara watapata fursa ya kukutana na Wanunuzi wa huduma hizo ana kwa ana kupitia Tamasha hilo, ” alisema Balozi Amina .
Waziri Amina amefahamisha kuwa ukuaji wa Sekta ya Biashara ndio chanzo cha kuongeza ajira nchini na kunyanyua pato la mwananchi na uchumi wa Nchi kwa Ujumla
Wakati huo huo amesema Tamasha hilo litaambatana na uzinduzi wa kliniki ya biashara yenye lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za papo kwa papo na kutatua changamoto zinazowakabili Wafanya Biashara katika uwendeshaji wa Biashara zao
Amefahamisha mafanikio mengi yaliopatikana katika matamasha yaliyopita ambapo kwa mwaka 2019 walipata jumla ya washiriki 290 kutoka nje ya nchi na ndani ya nchi jambo ambalo limepelekea ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma kulinganisha na maonesho ya mwaka juzi 2018
Sambamba na hayo amesema Tamasha hilo litatoa siku maalum kwa Vijana kutangaza masuala ya ubunifu ili kuweza kupunguza tatizo la ajira hapa nchini
Kauli mbiu ya Tamasha la sita la Biashara Zanzibar ni “Maendeleo ya Viwanda ni chachu ya ajira kwa Vijana “ likienda sambamba na Shamrashamra za Maadhimisho ya sherehe ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar .