Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jaffo amewataka wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo China kuwekeza nchini ili kukuza uchumi na kutoa ajira kwa vijana jambo ambalo litaleta tija kwa Taifa.
Akizungumza leo Julai,6 2024 wakati alipohudhuria Siku maalum ya China iliyoambatana na maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa – Sabasaba yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Dkt. Jaffo amesema kuwa Tanzania na China zinauhusiano wa muda mrefu ambayo yemeleta faidi katika nchi hizo hasa katika uchumi kwa kusafirisha bidhaa.
“Uhusiano mwingine upo kwenye viwanda vya wachina ambavyo vimejengwa hapa nchini na kutoa ajira, ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa kufanya kazi ya ukandarasi” amesema Dkt. Jaffo.
Dkt. Jaffo amesema kuwa uwepo wa wawekezaji nchini itasaidia kuimarika kwa sekta binafsi kwa kusaidia kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya juu nchini.
Amefafanua kuwa taarifa inaonesha kwamba zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.3 tunasafirisha , lakini tunaingiza bidhaa kutoka China ambazo thamani yake ni zaidi ya shilingi trilioni 3.5..
Dk. Jaffo amehamasisha kuendelea kwa ushirikiano huo na kuwekeza ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana, kwani vijana wengi wanamaliza vyuo vikuu ambapo serikali haiwezi kutoa ajira kwa watu wote.
Amesema kampuni 100 zimeweza kushiriki katika maonesho hayo ua 48 ya biashara ya kimataifa.
“Makampuni hayo yametoka China, hii tunavutia uwekezaji katika nchi yetu, binafsi kama Serikali imeamua inaweka mazingira wezeshi kuhakikisha wawekwzaji wanapata fursa ya kuwekeza nchini,” amesema Dkt. Jaffo.