Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Rutuba akitoa maelekezo kwa  wataalam wa benki hiyo wakati alipotembelea banda lake kwenye maonesho ya biashara ya 48 yanayoendelea kwenye viwanja vya maonesho vya Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam Julai 6, 2024.

……………………… 

NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea na utekelezaji wa upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha kwa kutengeneza mitaala ambayo itamwezesha kila mwananchi kupata elimu ya fedha ambayo itamsaidia kufanya uwekezaji na kuleta tija kwa familia na Taifa.

Akizungumza leo Julai 6, 2024 baada ya kutembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya Biashara ya 48 ya Kimataifa yanayofanyika katika Viwanja vya sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema kuwa wameweka mifumo jumuishi ili watanzania wafikiwe na huduma ya fedha kwani ni haki ya msingi ya kila mwananchi.

Tutuba amesema kuwa watu wengi wamehamasika kufika katika banda la BoT kupata elimu ikiwemo usimamizi wa uchumi kupitia sera ya fedha kwa kutumia riba ya benki kuu.

Amesema kuwa hali ya uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa nzuri kutokana na usimamizi mzuri, hivyo kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2023 ulikuwa kwa asilimia 5.1.
“Kadri muda unavyozidi kwenda hali ya uchumi itaendelea kuwa nzuri na kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa gharama stamilivu” amesema Gavana Tutuba.

Amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu ya fedha pamoja na kutoa tahadhari kwa watu wasiendelee kukopa katika makampuni ambayo hayana kibali cha kufanya kazi ya kutoa mikopo.

Gavana Tutuba amesema kuwa wapo baadhi ya watu wamekiuka misingi na taratibu ambazo zimewekwa na BoT hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Amefafanua wapo katika mpango wa kuuza hati fungani na dhamana za serikali kwani ni uwekezaji wa uhakika ambapo hakuna siku BoT watashindwa kulipa faida au mtaji uliowekezwa.
“BoT imepewa dhamana ya kuchapisha au kusambaza fedha hivyo hakuna siku itashindwa kulipa dhamana yako kwa sababu kila siku inakusanya mapato na inakuwa na uwezo wa kulipa madeni pamoja na riba” amesema Gavana Tutuba.

Amesema kuwa huduma ya kifedha ni haki ya msingi ya kila mtu hivyo ni muhimu kila mtanzania kupata elimu hiyo kwa kutumia mitaala tofauti.

Katika Maonesho ya Biashara ya 48 ya Kimataifa BoT inaendelea kutoa elimu katika maeneo tofauti ikiwemo Fedha, Uwekezaji, Masoko ya fedha, kuwezesha upatikanaji wa fedha Jumuishi, Utawala na huduma za Chuo cha Benki.