Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 55 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) akimpongeza mhitimu aliyekuwa na mahitaji maalum aliyefanikiwa kuhitimu na kufaulu vizuri licha ya kuwa na ulemavu wa kuona katika mahafali yaliyofanyika 06.12.2019 Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia , Dkt. Leonard Akwilapo ( wa tatu kushoto waliokaa), akifuatiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Naomi Katunzi , Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya watu Wazima (TEWW), Dkt. Michael Ng’umbi (wa tatu kulia waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakufunzi wa TEWW walioshiriki kwenye Mahafali ya 55 ya TEWW yaliyofanyika Jijini Dar es Salaaam tarehe 6/12/2019
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Michael Ng’umbi akizungumza wa wahitimu (hawapo pichani) wakati wa Mahafali ya 55 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, yaliyofanyika tarehe 06.12.2019 jijini Dar es Salaam
(Picha zote na TEWW)
………………
Na Mwandishi wetu
Wanafunzi 913 wahitimu masomo yao katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa mwaka wa masomo 2018/2019.
Akizungumza wakati wa mhafali ya Taasisi hiyo yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Katibu mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amesema kuwa kati ya wanafunzi hao 138 ni wa shahada, 724 ni stashahada na 50 ni wa astashahada.
“ Idadi ya wahitimu kwa mwaka 2018/2019 ni sawa na ongezeko la asilimia 32% ikilinganishwa na 690 kwa mwaka 2017/2018”; Alisisitiza Dkt. Akwilapo
Akifafanua amesema wahitimu hao wanatoka Kampasi za Dar es Salaam, WAMO Morogoro na Luchelele Jijini Mwanza wanawake wakiwa 565 na wanaume 397.
Pia Dkt. Akwilapo amewaasa wahitimu hao kuzingatia weledi na taaluma waliyopata katika kuchangia maendeleo ya Taifa kwa kufuata sheria kanuni na taratibu zilizopo kwa maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi hiyo Dkt. Naomi Katunzi amesema kuwa udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 4,598 katika mwaka wa masomo 2018/2019 na kufikia wanafunzi 7,042 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 75.
Aliongeza kuwa ongezeko hilo litachangia kuongeza mapato ya ndani ya Taasisi hiyo yatakayosaidia katika shughuli za uendeshaji na kuongeza tija.
Naye mkurugenzi mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Michael Ng’umbi amesema kuwa wamekuwa wakishirikiana na wadau wa maendeleo kutekeleza programu iliyojikita katika kujenga stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), Pamoja na stadi za maisha ya ujasiriamali ambapo wanufaika 961 wamefikiwa na mradi huo.
Vilevile wasichana 627 wamenufaika na mradi wa elimu ya Sekondari kwa wasichana walio nje ya shule katika mkoa wa Tanga ikiwa ni sehemu ya juhudi za TEWW kuchangia katika kukuza kiwango cha elimu hapa nchini na kupunguza idadi ya wanaokosa fursa ya elimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.
Aidha, Dkt. Ng’umbi amesema kuwa TEWW ina jukumu la kushirikiana na wadau binafsi kuwapatia elimu watoto, na vijana takribani milioni 3.5 waliokatisha masomo kwa sababu za utoro na mimba ili waweze kutoa mchango katika kukuza uchumi kupitia shughuli za uzalishaji.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imekuwa ikishirikiana na wadau kama UNESCO na KOICA kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kukuza kiwango cha elimu na kuyawezesha makundi maalum kama wasichana walikosa elimu katika mfumo rasmi kwa sababu mbalimbali.