NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
BODI ya Barabara ya Mkoa wa Pwani, imeelekeza, kupitiwa upya kwa mkataba wa mkandarasi wa barabara ya Tamco Kibaha kwenda Mapinga wilayani Bagamoyo ( kampuni ya Skol) ambae anaonekana kusuasua kuanza ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo.
Wakizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo, baadhi ya wajumbe walisema, wanashangaa kuona mkandarasi huyo tangu apewe kazi hakuna alichokifanya .
Akizungumza kwenye kikao hicho, mkuu wa mkoa Mhandisi Evarist Ndikilo alieleza kutokana na wajumbe kutoa malalamiko juu ya kampuni mbili za Skol na Southen Link ni vema wakala wa Barabara Nchi Tanroads kuliangalia kwa kina suala hilo.
Ndikilo alibainisha, kuna haja sasa ya mkataba wake kuangaliwa ikiwezekana kazi hiyo ipewe kampuni nyingine ili iendelee na ujenzi huo kutokana na kampuni hiyo kutoonyesha uwezo.
“Nitafanya ziara kutembelea ujenzi wa barabara hiyo ili kujionea hali halisi ya ujenzi huo ambapo ujenzi huo wa kilometa tano zimepewa kampuni hizo lakini kipande walichopewa kampuni hiyo ya Skol bado hakijajengwa kabisa,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema,ucheleweshaji wa ujenzi huo itachelewesha utekelezaji wa muda wa ujenzi wa mradi huo ambao unajengwa kwa awamu.
Naye meneja wa Wakala wa barabara Tanroads mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas Msangi alisema kuwa kwa sasa wamewasiliana na makao makuu yao kupitia kitengo cha masuala ya kisheria ili kuangalia mkataba huo ikiwezekana wavunje mkataba huo.
Msangi alisema kuwa tayari wamemuandikia barua nne kuhusiana na uwezo wake lakini inaonyesha kama kuna tatizo hivyo wanaendelea na hatua mbalimbali ili kumalizana naye.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa barabara hiyo ni muhimu sana kwani inaunganisha wilaya za Kibaha na Bagamoyo.
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa barabara hiyo ni mbaya kwani imeharibika kwa kiasi kikubwa hivyo ni vema wakandarasi hao wakaongeza nguvu ili kukamilisha ujenzi huo.