Kongamano la Ukombozi wa Maombi ya Tanzania limefanyika katika viwanja vya Nyerere Square likiwa na lengo la kumuomba Mungu kukomboa taifa dhidi ya matatizo ya ushoga, ulawiti, usagaji huku watumishi wa Mungu pamoja na vikundi vya kusifu na kuabudu vikiwepo kuwasaidia na kuwaombea wenye shida mbalimbali.
Akizungumza katika kongamano hilo jijini Dodoma mkuu wa wilaya ya Chemba Gerald Mongella amesema wazazi pamoja na walezi wameahidiwa ufalme wa Mungu kutokana na matendo yao lakini watoto wamehaidiwa ufalme huo kutokana na utoto wao, hivyo wazazi na walezi hawapaswi kunya’ganya mtoto haki na fursa aliyoahidiwa na mwenyezi Mungu.
“Watoto sio wa kunyanyaswa bali tujitahidi kuwapa baraka zetu kwani kwasasa tumeingiliwa na huu utandawazi hasa janga la ushoga, usagaji, ubakaji na kadhalika na hili jambo ni lazima tujikusanye wote tuanze kupambana nalo,”
Mongella ameongeza kuwa, “Binafsi ombi langu ni kwamba tuhakikishe tunapambana sana kuzuia unyanyasaji unaomtesa mtoto kwasababu kitaalamu inaonyesha mtoto akipata unyanyasaji huo ni mara chache sana hurudi kisaikolojia sawasawa, mara nyingi huwa ina waasili kisaikolojia na kuwapelekea kwenda kuwa binadamu wasiofaa.”
Aidha amesema Timotheo 2:3 inaeleza jinsi mwisho wa dunia ulivyokaribia kwani yale mengi yaliyotajwa ndiyo yanatokea katika ulimwengu wa sasa hivyo watumishi, wazazi na walezi wanapaswa kupambana usiku na mchana kuhakikisha vita hiyo wanaishinda.
Pia Mongella amesisitiza haki za watoto zilindwe ikiwa kucheza salama, elimu pamoja na wajibu wa kupewa upendo pamoja na kuhimiza wazazi pamoja na walezi kuwa na moyo wa kutoa taarifa za matendo wanayofanyiwa watoto ikiwa na kutoa taarifa za viashiria katika vyombo vya sheria ili kukinga matendo ya uovu.
Kwa upande wake Askofu wa kanisa la G.F.C Malaki Solo amesema taifa lina viongozi wazuri hivyo linapaswa kubadilika kwani serikali ina maadili ya watumishi wake hivyo mchungaji au askofu asipokemea janga la ushoga na usagaji hapaswi kuchunga kondoo wa bwana.
Amesema viongozi wa dini katika mkoa wa Dodoma wamefanya vyema kukusanyika na kuomba katika makao makuu ya nchi kwani mkoa huo umebeba roho nyingi za watu wa makabila na mataifa tofauti.
“Kitabu kile cha Matayo 16:18 kinasema nitalijenga kanisa langu wala milango ya kuzimu haitalishinda, kwaio tupo mahali hapa tunajua kwamba kanisa haliwezi kushindwa na kuanzia hapa tunaanza kuwasha moto na jambo hili liwe ni taarifa kwa nchi nzima,”
Solo amesema ajenda hiyo ya kitaifa linapaswa liangaliwe na kwa muelekeo mtambuka iweze kukomesha, kukwamisha na pia kuendela kupaza sauti kwa wazazi, watoto na vijana kuepuka na kulilinda taifa liwe na maadili mema.
Pia amesisitiza serikali iendelee kupinga maombi ya kusajili ushoga Tanzania ili kulinda masilahi ya taifa, utamaduni, maisha ya watoto pamoja na hatima ya wasomi wa Tanzania.