Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2924 Godfrey Mnzava,akimsikiliza meneja wa Tarura wilaya ya Namtumbo Mhandisi Fabian Lugalaba kuhusu ujenzi wa barabara za lami za mitaa katika mji wa Namtumbo jana,kulia Mkuu wa wilaya hiyo Ngollo Malenya.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Godfrey Mnzava wa tatu kulia,akikagua barabara la ya lami katika mji wa Namtumbo mkoani Ruvuma jana,kulia kwake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya,wa pili kulia Meneja wa Tarura wilayani humo Fabian Lugalaba na wa kwanza kulia mratibu wa Mwenge mkoa wa Ruvuma Joel Mbewa.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2924 Godfrey Mnzava kushoto,akiondoa kitambaa kuashiria ufunguzi wa barabara ya lami za mitaa katika MJi wa Namtumbo mkoani Ruvuma jana,kulia Mkuu wa wilaya hiyo Ngollo Malenya.
Mkazi wa mji wa Namtumbo mkoani Ruvuma Mustafa Njiwa,akimpa baraka Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2924 Godfrey Mnzava, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo.
Na Mwandishi Maalum,Namtumbo
WAKALA wa barabara za mijini na vijijini(TARURA)umeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa barabara za lami za mitaa katika mji wa Namtumbo mkoani Ruvuma, ili kuondoa kero ya usafiri na kurahisisha shughuli za usafirishaji hasa katika kipindi cha masika.
Hayo yamesemwa jana na Meneja wa Tarura wilaya ya Namtumbo Mhandisi Fabian Lugalaba kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava wakati wa mbio za Mwenge wilayani humo.
Alisema,ujenzi wa barabara za lami Namtumbo mjini zenye urefu wa kilometa 1.6 umetekelezwa kupitia fedha za mfuko wa barabara kwa kumtumia Mkandarasi Luke Associates Ltd ambao utekeleza wake ulianza mwezi Disemba 2022 na kukamilika mwezi Juni 2023.
Lugalaba alisema,kwa sasa Tarura imekamilisha ujenzi wa barabara tatu za mitaa ambazo ni Namtumbo-Shule-Bomani yenye urefu wa kilometa 1.3, Njau Njau-Mpunga Shop yanye urefu wa mita 170 na barabara ya Kanduru-Kambanga urefu wa mita 170.
Kwa mujibu wa Lugalaba,madhumuni makubwa ya ujenzi wa barabara za lami katika mji wa Namtumbo ni kuimarisha mawasiliano kati ya kitongoji cha Namtumbo na Bomani na kuboresha mandhari ya mji huo.
Alisema,mradi wa ujenzi wa barabara hizo umegharimu jumla ya Sh.milioni 889,998,200 na umehusisha ujenzi wa matabaka ya changarawe,lami nyepesi na kokoto.
Ametaja kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na uwekaji wat aa 43 za sola barabarani,kujenga makalavati mita 101,uwekezaji wa alama za barabarani 10 na kujenga mifereji urefu wa mita za mraba 3,084.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha miundombinu ya barabara za mijini na vijijini hapa nchini.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 Godfrey Mnzava,amewapongeza wataalam wa Tarura ngazi ya wilaya na Mkoa wa Ruvuma kwa kufuata sheria za manunuzi ya umma wakati wa kumpata mkandarasi aliyejenga barabara hiyo.
Mnzava,amewataka wakuu wa taasisi na idara zote za Serikali mkoani Ruvuma kuhakikisha wanafuata sheria kwa kuwashindanisha watoa huduma hususani wakandarasi wanapotaka kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuepusha malalamiko yasiokuwa ya lazima.
Mkazi wa Namtumbo Mjini Ali Ngonyani,ameipongeza Tarura kwa ujenzi wa barabara za lami,kwani zimesaidia sana kuboresha mazingira na kurahisisha mawasiliano kutoka sehemu moja na nyingine.
Hata hivyo,ameiomba serikali kuendelea kuipatia fedha Tarura ili iweze kujenga barabara nyingi zaidi za lami kwa kuwa mji wa Namtumbo bado kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa barabara za lami.