KUTOKANA na kuongeza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi shirika lisilo la kiserikali la Nachingwea Paralegal Aid Organization (NAPAO) imeamua kutoa elimu ya sheria ya mtoto kwa wananchi wa kijiji cha Mkonjela Chini ili jamii itambue haki za mtoto na wajibu wao katika malezi ya mtoto.
Akizungumza na wazazi kuelekea siku ya mtoto wa Afrika Mkurugenzi wa Shirika hilo lisilo la kiserekali ambaye ni msaidizi wa kisheria,Sabrina Dossa alisema kuwa wazazi lazima watambue haki za mtoto kama vile kumpa ulinzi,elimu na kumpa mahitaji yote muhimu kwa mtoto.
Dossa alisema kuwa wazazi wanapaswa kufichua matendo yote ya ukatili wa kijinsia,kama vile ulawiti, ubakaji na ndoa za utotoni ili kuwa na kizazi bora kwa faida ya familia na Taifa kwa ujumla.
Aliwataka wazazi ,walezi na jamii kuwa makini katika malezi kwa kuwafunza watoto Mila na tamaduni zao na kuwapatia mafundisho yenye maadili mema kwa jamii na maisha yao kwa ujumla.
Kwa upande wake afisa habari na mawasiliano wa kiserikali la Nachingwea Paralegal Aid Organization (NAPAO), Christopher Lilai alieleza kuwa shirika niatoa msaada kisheria,ushauri wa kisheria kwa jamii pamoja na usuluhishaji wa migogoro kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kifedha wa kugharamia.
“Shirika letu litoa huduma za kisheria bila malipo yeyote kwa wale ambao hawana uwezo lengo ni kumfanya mwananchi apate haki yake bila kuathiriwa na umaskini”alisema Lilai.
Hivyo alitoa wito kwa kila mwananchi anaehitaji msaada huo kufika katika ofisi zao au kwa wasaidizi wa kisheria waliopo kwenye kata 14.
Naye mmoja wa wazazi, wa kijijini hapo Zuhura Ungele ameeleza kuwa bahadhi ya wazazi wanawagopa watoto wao wanaosoma sekondari hivyo kufanya watoto wengi huwadharau wazazi wao pindi wanapofikia elimu ya kidato cha nne (4) na kuendelea madai ya kujiona wao ni wasomi kuliko wazazi wao .
Hivyo kuelekea siku ya mtoto wa Afrika aliwataka watoto kujifunza na kuelewa thamani ya mzazi katika jamii
Ungele alisema kuwa mwenendo wa maisha ya watoto wa siku hizi si mazuri kwani kwa asilimia kubwa yanakiuka maadili ya watanzania na kuwataka watoto wote kuanza kuwajibika kwa wazazi wao ili wapate malezi bora na mema kwa maisha yao.