Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wametakiwa kusaidia jamii inayowazunguka (CSR) ili kutimiza takwa la kisheria.
Ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya ameyasema hayo juzi wakati mkurugenzi wa kampuni ya Heroes mining camp Basil Roman Njau akikabidhi vyakula kwa yatima wa eneo hilo.
Mgaya amesema sheria inawataka wachimbaji kusaidia jamii inayowazunguka kwa kutoa kiasi cha mapato yao ila wachimbaji wengi wao hawafanyi hivyo pindi wanapopata.
Amesema sheria inawataka wachimbaji kufanya hivyo kwani shughuli za uchimbaji zitakuwa zimewanyima baadhi ya fursa wenyeji hivyo wanapaswa kuangaliwa.
“Tunaipongeza kampuni ya Heroes mining camp kupitia mkurugenzi wake Basil Roman Njau kwani bado hawajaanza uzalishaji ila wametumia Sh2 milioni kusaidia yatima,” amesema.
Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Saidia Wanajamii Tanzania (SAWATA) lililoandaa na kuratibu shughuli hiyo Mohamed Issa Mghanja ameipongeza kampuni ya seneta Basil Roman Njau kwa kutoa msaada huo.
Mghanja amesema kupitia Sawata wamewashirikisha wenyeviti wa vitongoji ili kupata yatima wenye uhitaji halisi.
Katibu wa SAWATA, Mohamed Shauri amesema mkurugenzi huyo amefanya jambo jema kwani nyumba yenye yatima malaika wanaiona ikiwa imewaka taa.
Kwa upande mkurugenzi wa kampuni ya Heroes mining camp, Basil Roman Njau amesema amewiwa kutoa kiasi hicho kidogo ili kusaidia jamii ya eneo hilo.
“Bado madini hayajatoka tumeona mimi na familia yangu tutoe sadaka kwa yatima na nawaahidi tukifanikiwa kwenye uzalishaji tutawasaidia mitaji wajane hawa ili wahudumie vyema familia zao,” amesema Njau.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema sadaka iliyotolewa na kampuni hiyo imegusa wahitaji halisi hivyo wanaipongeza.
“Kwa sababu mmetoa sadaka hata kabla ya uzalishaji kutokea, Mungu hawezi kuwaacha hivi hivi kwani dua na sala za yatima zitakuwa juu yenu,” amesema Kobelo.
Makamu Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Christopher Chengula ameupongeza uongozi wa kampuni ya Heroes mining camp kwa kutoa msaada huo kwa wahitaji.