Na Sophia Kinginali.
TUME ya Ushindani (FCC) na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji katika kuboresha mazingira ya uwekezaji wa viwanda na kudhibiti uzalishaji wa bidhaa bandia.
Hayo yamesemwa leo Juni 5,2024 jijini Dar es Salaam, baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema lengo la kusaini makubaliano hayo ni kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi kukuza viwanda na kudhibiti bidhaa bandia.
“Kusainiwa wa makubaliano haya kutawezesha kufikia malengo ya serikali ya Rais Dk.Samia ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.Mahusiano haya yatahusu namna bora ya kubadilishana taarifa hususan utekelezaji wa sheria mbili ambazo FCC tunazisimamia ikiwemo ya Ushindani na ya alama au nembo ya bidhaa zinazowahusu wenye viwanda,” amesema.
Amesema katika majukumu ya CTI kupitia sera na dira zao zinaonyesha ambavyo wanalenga kulinda mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini kwa wenye viwanda kufikia matarajio yao na kukuza uchumi wa viwanda.
Aidha Erio, amesema wanaendelea kulinda na kushabihisha ushindani, hivyo wanahakikisha wanadhibiti vitu ambavyo vinaweza kuathiri wawekezaji hao ikiwemo ukiukaji wa sheria na makubaliano kuhakikisha havifanyiki.
Akielezea kuhusu sheria ya bidhaa bandia amesema, inazuia kupitia mipaka ya nchi na kutozalishwa nchini, ndiyo maana wamesaini makubaliano hayo kuhakikisha wanalinda uzalishaji huo wenye tija katika kukuza ajira, fursa ya uchaguzi wa bidhaa na kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye viwanda Nchini (CTI), Mhandisi Leodgar Tenga, ameipongeza FCC kwa kufanikisha kusainiwa kwa makubaliano hayo yanayotokana na ushirikiano mzuri wa Taasisi hizo mbili.
Amesema kufanikiwa kwa makubaliano hayo ni fursa kubwa ya kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji wa viwanda yanalindwa na kufikia azma ya serikali ya sekta hiyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mkurugenzi Erio amesema kupitia CTI, watakubaliana wao kuwa na umoja wao uliosajiliwa wa kulinda nembo za bidhaa zao zisiibiwe na kutumia na wengine bila kibali, akitolea mafanikio kwa mataifa yaliyoendelea ikwemo Marekani walivyofanikiwa katika hilo.