Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akitoka kukagua ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji wa Izizimba A katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akimsikiliza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kwimba akitoa maelezo kuhusu Mradi wa Maji wa Isunga-Kadashi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akielezea hatua ya ujenzi iliyofikiwa kwenye Mradi wa Maji wa Ngudu kwa Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wilayani Kwimba, mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiangalia mita ya pampu itakayosukuma maji kwa Mradi wa Maji wa Isunga-Kadashi, wilayani Kwimba, mkoani Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (katikati) alipokuwa kwenye Mradi wa Maji wa Izizimba A, mkoani Mwanza.
………………….
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutekeleza miradi ya maji na kumaliza tatizo la maji kwa wananchi kwa wakati.
Aweso ametoa maelekezo hayo alipotembelea na kukagua miradi ya maji ya Izizimba A, Ngudu na Isunga-Kadashi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na kubaini changamoto ya utaratibu wa manunuzi kuchukua muda mrefu na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa maji vijijini.
Naibu Waziri Aweso amewataka maafisa ugavi wasiwe kikwazo katika kutekeleza miradi ya maji, huku akiwahakikishia wakazi wa Kijiji cha Izizimba A kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itamaliza kero yao na itaendelea kutekeleza miradi ya maji yenye viwango na kwa wakati ili kutimiza adhma ya Rais Dkt. Magufuli ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema katika kutatua changamoto ya mabomba kwenye Mradi wa Izizimba A, watafanya malipo ya ununuzi wa mabomba kwa Kampuni ya PLASCO wiki ijayo kwa ajili ya kuleta mabomba yanayohitajika kukamilisha mradi huo.
Akisisitiza kuwa wizara imelenga kuharakisha hatua zote za utekelezaji wa miradi wa maji ikiwemo upembuzi yakinifu, usanifu, upatikanaji wa wakandarasi na manunuzi ili miradi ya maji iweze kukamilika haraka iwezekanavyo.
Naibu Waziri Aweso amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku nne ya kutembelea na kukagua miradi ya maji mkoani Mwanza, ambapo Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 282 kwa mkoa huo katika kuhakikisha inamaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.