MUONEKANO wa jengo jipya la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambalo lipo katika hatua za umaliziaji ambapo serikali imetoa shilingi bilioni 3.3 kutekeleza mradi huo.
….
Na Albano Midelo,Mbinga
Serikali imetoa shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Joseph Rwiza wakati anatoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ambaye amefanya ziara ya kukagua miradi katika wilaya ya Mbinga.
Rwiza amesema hadi sasa Halmashauri hiyo imepokea shilingi bilioni 3.3 ambazo zimepokelewa kwa awamu nne na kwamba mradi upo katika hatua za umaliziaji.
“Wananchi wa Mbinga wanaipongeza serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi za kuboresha utendaji kazi katika sekta ya umma ili kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma karibu na kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa wafanyakazi’’,alisema Rwiza.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameuagiza uongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanaboresha mazingira ya jengo hilo ikiwemo kupanda miti ya matunda na kivuli ili eneo hilo liwe na madhari ya kuvutia.
Amesema serikali imetoa mabilioni ya fedha za walipa kodi katika kutekeleza mradi huo hivyo ni vema majengo hayo kutunzwa ambapo amewapongeza kwa usimamizi mzuri wa jengo hilo ambalo limejengwa kwa ubora mkubwa.