Wadau wa kilimo katika wilaya ya Songea  wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Michael Mbano wakiwa kwenye zoezi la uvunaji viazi mviringo katika shamba  darasa eneo la Shule ya Tanga  mjini Songea.
Baadhi ya viazi mviringo vilivyovunwa katika shamba darasa la Shule ya Tanga Manispaa ya Songea.
Mgeni rasmi kwenye zoezi la uvunaji viazi mviringo katika shamba darasa la Kata ya Tanga Manispaa ya Songea ambaye ni Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mheshimiwa Michael Mbano akiangalia viazi mviringo vilivyovunwa katika shamba darasa hilo.
Baadhi ya wananchi kutoka wilaya ya Songea ambao ni wakulima wakiwa kwenye hafla ya zoezi la uvunaji wa viazi mviringo katika shamba darasa la Shule ya Tanga mjini Songea
………

Na Albano Midelo,Songea

UTAFITI uliofanyika na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) katika Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kuanzia mwaka  2020 hadi 2024 umebaini kuwa viazi mviringo vimetoa matokeo mazuri katika uzalishaji.

Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Mpuya  akizungumza kwenye zoezi la kuzindua uvunaji wa zao la viazi mviringo katika shamba darasa la majaribio Kata ya Tanga Manispaa ya Songea ya Songea, amesema  SAGCOT wamefanya utafiti wa kulima viazi mviringo katika vijiji vya Liganga,Mang’ua na Tanga wilayani Songea  na zao hilo kuonesha mafanikio makubwa katika uzalishaji.

“Watu wengi wanaamini viazi mviringo vinastawi  vizuri mkoani Njombe na hata mimi nilikuwa naamini hivyo,kumbe kama huna utafiti huna haki ya kusema,utafiti wetu wilayani Songea umebaini viazi mviringo vinafanya vizuri sana’’,alisisitiza Mpuya.

Ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuona fursa ya kutengeneza uchumi na kuongeza kipato kupitia zao la viazi mviringo ambapo utafiti umebaini kuwa heka moja ya viazi mviringo inazalisha magunia 200 hivyo kumuingizia mkulima wastani wa shilingi milioni 16.

Amesema Idara ya kilimo Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na SAGCOT inahamasisha kilimo cha parachichi katika  Mkoa wa Ruvuma ambapo hadi sasa  kuna Zaidi ya hekari 500 ambazo zimepandwa parachichi ambazo  ambazo huanza kuzaa baada ya miaka mitatu.

Mgeni rasmi kwenye hafla ya uvunaji viazi mviringo,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Michael Mbano amesema wakulima wa Songea kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea zao moja la mahindi ambapo  amesema zao la parachichi na viazi mviringo linakwenda kuleta fursa mpya na  tija kwa wakulima.

Mbano amesisitiza kuwa wakati anapata taarifa za uzinduzi uvunaji viazi mviringo hakuamini kama ardhi ya Songea inafaa kwa kilimo cha zao hilo na kwamba wananchi wengi wa Songea hawana taarifa kama viazi mviringo vinaweza kustawi na kuwaongezea kipato.

Amesema  tani 20 za viazi mviringo ambazo zinavunwa kwa hekari moja  ni uchumi ambao kila mwananchi wa Mkoa wa Ruvuma anatamani kupata ambapo pia ametoa rai kwa wananchi wa Songea kulima zao la parachichi ambalo pia linatoa kipato kikubwa

Amesema utafiti umebaini mti mmoja wa parachichi kwa mwaka unaweza kumuingia mkulima kati ya shilingi 500,000 hadi 800,000 hivyo ametoa rai kwa wananchi wa Manispaa ya Songea  kupanda miti ya matunda kama parachichi  na viazi mviringo ili kukuza uchumi wao.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima cha LUSITU AGRI BUSSINESS ambaye pia ni Mkulima  Mwezeshaji Beno Mgaya ameitaja Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) imedhamiria kutoa mafunzo ya kilimo biashara ili wakulima waweze kujitambua kwa kuhamasisha kilimo cha parachichi na viazi mviringo katika Mkoa wa Ruvuma.

Amesema utafiti walioufanya katika wilaya ya Songea kuhusu zao la viazi mviringo kwa kutumia mbegu za aina mbili kutoka nchini Uholanzi  zimetoa matokeo mazuri na kwamba hapa nchini hivi sasa kuna aina 16  za mbegu za viazi mviringo.

Mgaya amelitaja lengo la kuanzisha kilimo cha viazi mviringo ni kumwezesha mkulima kupata kipato wakati anasubiri zao la parachichi ambalo huchukua miaka  mitatu hadi kuanza kuzaa mkoani Ruvuma.

Amesema SAGCOT imedhamiria kuwa na mashamba darasa katika zao la viazi mviringo katika maeneo ya Shule ya Tanga, Liganga,Litapwasi,Namatuhi na Peramiho wilayani Songea na kwamba mashamba darasa yote yapo katika mfumo wa umwagiliaji.

Hata hivyo amesema wakulima wa viazi mviringo mkoani Ruvuma wataweza kuzalisha kwa kutumia umwagiliaji hivyo kuzalisha  mwaka mzima na kumwezesha mkulima kupata kipato kizuri Zaidi.

Mwenyekiti huyo anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuiamini SAGCOT ili iweze kufanya kazi Tanzania nzima ambapo hadi sasa imeenea katika mikoa tisa. 

Kandidus Komba Mkulima Mwamasishaji kutoka Kijiji cha Liganga wilayani Songea, ameipongeza SAGCOT kwa kusimamia mradi huo kwa zao la  parachichi ambapo wakulima wa vijiji vya  Liganga, Peramiho,Litapwasi,Ndongosi,Lipokela, na Mang’ua,Mtakanini na Geraza la Kitai ,wamenufaika na mradi huo.