Mkurugenzi wa JK Cement Amit Kothari akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Hyatt jijini Dar es salaam leo mara baada ya kuingia makubaliano ya kibiashara na kampuni ya Gold Star ya jijini Dar es salaam.
Baadhi ya watendaji wa kampuni hizo wakiwa katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa JK Cement Amit Kothari akipongezana na Mkurugenzi Mtendaji wa Goldstar Bw. Srinivasan mara baada ya kusaini makubaliana ya kibiashara jijini Dar es salaam leo Kulia ni Pushpendra Singh.
Picha ya pamoja.
……………………………………
DIRA ya Serikali ya awamu ya tano ambayo imejikita katika ujenzi wa viwanda imezidi kuwavutia wawekezaji wengi zaidi wenye uhitaji wa kuwekeza na kutengeneza masoko zaidi nchini, ambapo leo Desemba 05 kampuni ya JK White cement (Afrika) Limited ambayo ni sehemu ya kampuni ya JK ya nchini India imetangaza rasmi kuungana kibiashara na kampuni ya uzalishaji wa rangi ya Goldstar Paints ya Tanzania ili kuingiza sokoni bidhaa mpya ya JK Wall Putty bidhaa ambayo ni poda laini itokanayo na saruji nyeupe yenye kutoa mwonekano mzuri kwa kuta na dari ambayo itaenda sambamba na mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa JK cement Amit Kothari amesema, ushirikiano huo wa kibiashara umelenga kukata kiu ya wananchi kwa kutoa bidhaa bora yenye kuendana na mazingira.
“JK Cement ni moja kati ya wazalishaji bora wa cement na tumepata washirika Makini ambao tutaziba ombwe lililopo pamoja na kutoa ajira, na kubwa zaidi ni kufungua ofisi na kupandisha bendera Tanzania kwa mara ya kwanza katika ukanda wa Afrika na dunia, na hiyo ni kutokana na ushirikiano mzuri tunaooneshwa na Serikali ya Tanzania” ameeleza Kothari.
Amesema kuwa wanajivunia kuwa sehemu ya watanzania na kueleza kuwa kampuni hiyo isiitwe ya wahindi bali watanzania kwa kuwa Goldstar Paint wamekuwa kwenye safari na dhamira ya kutoa bidhaa zenye ubora zenye kukidhi mahitaji ya watanzania kupitia bidhaa zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Goldstar Srinivasan amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele hasa katika masoko kwa Kuhakikisha kwamba inaleta bidhaa zenye viwango stahiki na kwa sasa wameongeza bidhaa nyingine kwenye soko jambo ambalo wanaamini litaleta mabadiliko na mapinduzi katika kuwahudumia wateja.
Amesema kuwa JK ikiwa moja kati ya kampuni kubwa za uzalishaji wa saruji nyeupe duniani na mzalishaji mkuu wa bidhaa ya Wall Putty nchini India wataendelea kuwahudumia watanzania kwa kuwapa bidhaa bora zaidi ambazo zinaendana na mazingira.
Kampuni ya JK cement yenye makazi yake Fujairah (UAE) wamekuwa wadau kwa nchi za Afrika na katika kujipapanua zaidi wamejiegemeza zaidi katika kukuza soko lake Tanzania kupitia muungano huo wa kibiashara na kampuni ya Goldstar iliyoanzishwa mwaka 1988 wamekuwa maarufu zaidi kupitia rangi ya Goldstar ambayo hupatikana kote nchini na ilichaguliwa miongoni mwa makampuni 50 bora zaidi nchini na TBS na TPSF mwaka 2017.