Kumekuwa na matukio mbalimbali ya uhalifu yanayotokea katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ambayo yanahusishwa na watoto ambao wanajulikana kwa jina maarufu kama “damu chafu”.
Ni kipindi cha miaka miwili sasa wananchi wamekuwa wakitoa malalamiko yao kwa vyombo vya usalama kuhusiana na matukio hayo.
Wahanga wakuu wa matukio hayo ni madereva wa bajaji na bodaboda, wanawake, wasichana na wafanyabiashara wadogo wanaochelewa kutoka kwenye biashara zao na kurudi nyumbani muda wa usiku kuanzia saa nne.
Katika kisa kilichotokea mtaa wa Nsemulwa dereva bajaji alinyang’anywa fedha mara baada ya kushusha abiria ambapo anadai kuwa alishtukia watoto wamezunguka bajaji huku wakitishia kumchoma kisu.
Licha ya kutuhumiwa kupora simu, fedha na mali za watu wanaotembea nyakati za usiku baadhi ya watoto hao pia wanadaiwa kuhusika katika kuvamia nyumba za watu, kwa kuingizwa kupitia madirisha na kufungua milango.
Aidha watoto hao pia wanadaiwa kuwa na tabia ya kuiba nguo zilizoanikwa baada ya kufuliwa, masufuria na majiko pale wanapokuta wenyeji wa kaya husika hawapo.
Kufuatia matukio hayo Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi limekuwa likiendesha misako ya mara kwa mara na kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na matukio ya uhalifu wakiwemo watoto wa umri wa miaka 7-14.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi S.A.C.P Kaster Ngonyani amesema kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2023, Jeshi hilo liliwakamata watoto 44 waliokiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya uhalifu.
Kamanda huyo wa Polisi ameeleza kuwa baada ya kukamatwa kwa watoto hao, walifanya mazungumzo na wazazi wao ambapo baadae watoto wao walitolewa kwa masharti ya mzazi na mtoto kufika kila siku asubuhi Polisi kuripoti.
Ameeleza kuwa zoezi hilo limesaidia watoto 24 wa miaka 7-8 kurejea kwenye masomo waliyokuwa wamekatisha ambao wengi wao ni darasa la kwanza hadi la tatu. Watoto wengine 20 wamechukuliwa na wazazi wao kwani walikuwa wakiishi kwa babu/bibi zao.
Aidha Jeshi la Polisi limekuwa na utaratibu wa kutembelea katika shule mbalimbali za msingi na kutoa elimu kwa wanafunzi ya namna ya kukataa kuhusika katika vitendo vya uhalifu.
Katika operesheni zilizofanyika baadhi ya vitu vilipatikana zikiwemo runinga, redio, mashine za michezo ya kubahatisha na baiskeli, ambapo pia watu wazima walitajwa kuwatumia watoto hao kufanya vitendo hivyo.
Watu wanne walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka yao na kesi zinaendelea.
Kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 sura ya 288 inakataza “kazi hatarishi” kwa mtoto ikiwa na maana ya kazi yoyote inayomuweka mtoto katika hatari ya kupata madhara ya kimwili au kiakili.
Mama mmoja mkazi wa Tulieni (jina linahifadhiwa) mwenye mtoto aliyekuwa anajihusisha na vitendo vya kihalifu anasema mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka nane alianza utoro wa shule, na baadae akawa hashindi nyumbani na wakati mwingine harudi kulala nyumbani.
Mama huyu anadai kuwa alipigiwa simu aende Polisi ambapo alimkuta mtoto wake na anaongeza kuwa kwa sasa mtoto anaendelea na shule na yupo darasa la pili.
Katika tukio jingine lililotokea mtaa wa Shanwe mtoto aliyedaiwa kuwa ni ‘damu chafu’ aliuwawa kwa kuchoma moto na watu wenye hasira, ambapo baba yake mzazi alithibitisha kuwa matendo ya mtoto wake yalikuwa hayafai.
Akizungumzia matukio hayo Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Bi. Jamila Yusuf amesema ni wajibu wa mzazi kuhakikisha anafuatilia matendo ya mtoto wake.
Amesema katika mikutano yake na jamii amekuwa akitoa rai kwa wazazi kuzingatia malezi bora.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatoa malezi timilifu kwa watoto hasa wa chini ya miaka nane na kuongeza kuwa watoto hawa ni rahisi kuwadhibiti.
“Kwanini tukose amani kwa sababu ya vibaka wadogo wadogo, hebu tukumbuke sisi tulilelewaje” alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Mpanda.
Askofu Ephraim Ntikabuze ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Lake Rukwa Development Organization la mkoani Katavi (LARDEO) ambalo linajishughulisha na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto, amesema jamii inapaswa kumlea mtoto katika mazingira yatakayofaa kumwezesha kujitegemea atakapokuwa mtu mzima.
Askofu Ntikabuze amelaani vitendo vya watoto kuhusishwa na matendo ya uhalifu kwani hayamjengi mtoto kuwa mtu muadilifu.
Bi. Tracy Salema ni Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Mpanda ameeleza kuwa kuwahusisha watoto katika vitendo vya uhalifu ni kuwanyima haki ya malezi stahiki pamoja na kuwavuruga kisaikolojia.
Ametaja madhara mengine ya mtoto aliyehusishwa na kazi za uhalifu kuwa ni kushindwa kukua kitimilifu na kuwa mkaidi.
Aidha mtoto huyo licha ya kuathirika kimwili na kiakili pia anapokuwa mtu mzima anaweza kuathirika zaidi kisaikolojia na huweza kujiingiza katika makundi ya wahalifu ama matumizi ya dawa za kulevya.
Mkakati wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya mwaka 2021/22 hadi 2025/26 inasisitiza ulinzi na usalama wa mtoto.
Hivyo basi kumuhusisha mtoto mwenye umri wa chini ya miaka nane katika matukio ya uhalifu ni hatari kubwa na uharibu ndoto za mtoto huyo.