Na.WAF, Dodoma
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeendelea kujiimarisha katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu mipakani kwa kutengeneza mfumo wa kukusanya na kutoa taarifa za wagonjwa wanaopatiwa rufaa za matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu maeneo ya mipaka ya nchi wanachama (Cross Border Referal System) ikiwa ni jitihada za kufikia malengo ya kidunia ya kutokomeza ugonjwa huu pindi ifikapo mwaka 2030.
Wagonjwa wa Kifua Kikuu sasa watapatiwa matibabu sambamba na kupatiwa huduma za ufuatiliaji na tathimini ya ufuasi wa dawa ili kuhakikisha wanamalizia matibabu yao kwa wakati wakiwa katika nchi hizo.
Hayo yamebainishwa leo Mei 21, 2024 na Mratibu wa Kitengo Huduma za Kinga na Matunzo Dkt. Allan Tarimo kutoka Mpango wa Taifa wa Kidhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Wizara ya Afya katika kikao kazi cha Wadau wa Huduma za Kifua Kikuu kwenye maeneo ya mipaka.
Dkt. Tarimo amesema tayari kuna mipaka 10 ambayo imeanza hatua za awali za kuingiza taarifa za wagonjwa wa Kifua Kikuu ambao wanaoingia na wanaotoka nchini ili waweze kupatiwa matibabu na ufuatiliaji matibabu yao vizuri.
Awali aneeleza kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na changamoto kubwa ya usimamizi wa matibabu na ufuatiliaji kwa wagonjwa katika maeneo ya mipakani kutokana muingiliano wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo ya mipakani.
Ameongeza kuwa malengo ya kikao kazi hicho ni kuwajengea uwezo wadau kuhusu mfumo huu mpya ili waweze kusimamia vizuri utekelezaji wake kwenye maeneo ya mipakani.
“Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu unatibika na kupona kabisa hivyo wagonjwa lazima wafuatiliwe katika kipindi chote cha matibabu ili kukamilisha matibabu,” amesema Dkt. Tarimo.
Vile vile amesema waanalenga kuhakikisha wadau wanabadilishana uzoefu ili mfumo huo uweze kwenda vizuri na kusaidia kufatilia matibabu ya wagonjwa kwa ufasaha.
Aidha kuhusu mifumo kusomana na ile ya ndani ya Nchi, Dkt. Tarimo amesema kuwa lengo la mfumo huu ni kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa katika maeneo mipakani na utajumuishwa pamoja na mifumo ya ndani ikiwemo mfumo wa wagonjwa wa Kifua Kikuu unaotumika ndani ya nchi ujilikanao kama DHIS2-ETL
Kikao hicho kimehudhuriwa na washiriki kutoka Wizara ya Afya, TAMISEMI, Wizara ya Kazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wadau wa Asasi za Kiraia katika maeneo ya mipaka pamoja na shirika la ECSA ambao ndio watekelezaji wakuu wa afua hii.