Mkurugenzi msaidizi Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana ajira na Watu wenye Ulemavu, Godfrey Chambu akizungumza kwenye Kongamano la uchumi kwa watu wenye ulemavu
Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Wilaya ya Nyamagana Hamza Nyamakurura akizungumza kwenye Kongamano la uchumi kwa watu wenye ulemavu
Mkurugenzi msaidizi Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana ajira na Watu wenye Ulemavu, Godfrey Chambu akizungumza kwenye Kongamano la uchumi kwa watu wenye ulemavu
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala akizungumza kwenye Kongamano la uchumi kwa watu wenye ulemavu.
Washiriki wa Kongamano wakiwa ukumbini
…………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza limeiomba Serikali kuwapa nafasi kwenye miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa likiwemo Soko kuu ili waweze kujiinua kiuchumi.
Ombi hilo lilitolewa Jana Mei 18, 2024 na Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Wilaya ya Nyamagana, Hamza Nyamakurura kwenye Kongamano la uchumi kwa watu wenye ulemavu lenye lengo la kuhakikisha kunakuwepo na utekelezaji wa haki za kazi na ajira kwa watu wenye ulemavu lililofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Jeshi Mkoani hapa.
Alisema watu wenye ulemavu wanapata changamoto kupata maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji mali hivyo mradi wa Soko kuu utakapokamilika wanaomba kupata nafasi katika eneo hilo hatua itakayosaidia kukuza fursa ya uchumi wao.
“Kongamano hili kinakaulimbiu isemayo “Hatutaki ombaomba, tunataka kazi” kazi inamuwezesha binadamu jujitegemea na kupata heshima katika jamii hivyo tunaomba sana Serikali iweze kusikia ombi letu”, alisema.
Akitoa mada ya haki ya kazi na ajira kwa watu wenye ulemavu Wakili wa kujitegemea, Remigius Mainde alisema sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 ibara ya 33 ibara ndogo ya tatu inasema kila mwajiri anaeweza kuajiri watu 20 ni lazima asilimia tatu wawe watu wenye ulemavu na atengeneze miundombinu itakayowawezesha kufanya kazi.
Alisema pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo bado Kuna baadhi ya waajiri hawafati utaratibu hivyo Serikali inatakiwa kutengeneza mfumo ili kuhakikisha sheria haivunjwi.
Kwaupande wake Mkurugenzi msaidizi Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu kazi vijana na ajira na watu wenyewe ulemavu, Godfrey Chambu alisema kwa sasa wanafanya mapitio ya sera ya Taifa ya huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 ili iendane na mazingira ya sasa.
Naye Mwenyekiti wa Idara ya wanawake na watoto Chama cha walemavu wa viungo Tanzania (CHAWATA), Janeth Maila alisema kwenye suala la ajira wamekuwa wakibaguliwa jambo ambalo limekuwa likiwaathili kisaikolojia.
“Tunashukuru leo kukutana kwenye Kongamano hili ambalo litatusaidia kukuza na kuongeza ufahamu kwa watu wenye ulemavu”, alisema Maila
Akizungumza kwenye Kongamano hilo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala, ametoa rai kwa watu wenye ulemavu kuzingatia taratibu na maagizo yanayotolewa katika uombaji wa ajira zinapokuwa zimetangazwa.
“Katika kuhakikisha suala la ajira kwa watu wenye ulemavu linapewa kipaumbele Serikali imeendelea kutoa nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu ambao wanakizi vigezo na wenye sifa, Serikali imeweka msisitizo kwa muombaji aweze kujieleza uleumavu alionao ili waweze kurahisisha uchambuaji wa maombi hayo lakini suala hili limekuwa ni changamoto hivyo kupeleka baadhi ya waombaji kukosa nafasi”, amesema Masala