Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe akiongoza kikao hicho cha majumuisho ya ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia wa kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa ERPP kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara Kilimo, Jijini Dodoma (Leo)
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe akiongoza kikao hicho cha majumuisho ya ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia wa kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa ERPP pamoja na Wajuumbe wa mkutano huo
Kiongozi Ujumbe wa Benki ya Dunia, uliokuwa ukiongozwa na Bwana Holger Kray, Mtaalam wa Masula ya Kilimo cha Kimkakati katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini pamoja na Bibi Sarah Simon Mwandamizi wa Masuala ya Kilimo Benki ya Dunia Tanzania
…………………
Na. Issa Sabuni-Wizara ya Kilimo, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe ameonya wakandarasi watatu waliopewa kazi ya kujenga miundombinu ya skimu za umwagiliaji katika mradi wa kuongeza tija na uzalishaji zao la mpunga (ERPP) mkoani Morogoro kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi mitatu ijayo.
Agizo hilo amelitoa jana(04.12.2019) wakati wa kikao cha tathmini ya miradi ya ukarabati wa skimu za umwagiliaji na maghala inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na wizara ya kilimo kilichofanyika ukumbi wa wizara Jijini Dodoma..
“Ili kuhakikisha miradi hii inakamilika ndani ya muda mfupi,naagiza mratibu wa mradi huu January Kayumbe kutokwenda mapumziko mwisho wa mwaka hadi wakandarasi hawa waliozembea wakamilishe miradi kabla ifikiapo Aprili 2020” alisema Mhandisi Mtigumwe.
Katibu Mkuu huyo amemtaka Mratibu wa Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa zao la Mpunga (Expanded Rice Production Project – ERPP) Mhandisi January Kayumbe kusimamia kwa ukaribu wakandarasi ili miradi ikamilike na kuwa na ubora unaokusudiwa na serikali.
Mhandisi Mtigumwe ametaja wakandarasi ambao hawajakamilisha kazi kuwa ni Lukolo Construction Company Ltd inayojenga miundombinu ya shamba la Mbegu la Msimba, lenye ukubwa wa hekta 640, linalomilikiwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA).
Pili, Kampuni ya Confits Company Ltd inayojenga miundombinu ya skimu ya umwagiliaji Msola Ujamaa Wilaya ya Kilombelo ambaye amefanya kazi kwa asilimia 25, na tatu Kampuni ya Goba Construction Ltd inayofanya kazi ya ujenzi wa miundombinu katika skimu ya Kigugu Wilaya ya Mvomelo imefanya kazi kwa asilimia 29.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo ameelezea mafanikio yaliyofikiwa na mradi huo tangu ulipoanza kuwa wakulima wa mpunga wamepata maarifa ya kilimo cha kisasa cha mpunga kulikosaidia kuongeza tija na uzalishaji.
“Mavuno ya mpunga yameongezeka kutoka tani 1.8 mwaka 2015/2016 na kufikia tani 5 hadi 6 kwa hekta mwaka 2018/2019 chini ya mradi wa ERPP “alisema Katibu Mkuu wizara ya Kilimo.
Kwa upande wake Mtaalam wa Masuala ya Kilimo cha Kimkakati katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Benki ya Dunia Bwana Holger Kray ameiomba Wizara kufanya ufuatiliaji wa karibu ili wakandarasi wa ujenzi skimu za umwagiliaji wakamilishe miradi hiyo ili wakulima wanufaike kwa uzalishaji kuongezeka pia kipato cha kaya na taifa.
Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa zao la Mpunga (ERPP) ulianza kutekelezwa mwaka 2015/2016 ambapo fedha kiasi cha dola za Marekani Milioni 22.9 zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji upande wa Tanzania Bara na Visiwani.