Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe,akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa majaribio wa wataalamu wa kujitolea kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na US Peace Corps ambao utatekelezwa katika wilaya za Bahi, Chamwino Mkoani Dodoma na Mafinga Mkoani Iringa,hafla hiyo imefanyika leo Mei 16,2024 jijini Dodoma.
Na.Mwandishi Wetu-Dodoma
Vijana 26 kutoka katika wilaya za Bahi, Chamwino na Mafinga wamechaguliwa kujiunga na mpango wa Majaribio wa Wataalamu wa Kitaifa wa kujitolea (National Volunteerism Pilot Program), mpango ambao umejikita katika kutoa elimu ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI na viashiria hatarishi kwa vijana kwa njia ya michezo katika vijiji vyao.
Mpango huo wa majaribio unaendeshwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na US Peace Corps ambao utahusisha jumla ya vijana 26 kati yao wasichana ni 13 na wavulana 13 waliochaguliwa katika vijiji vyao na kupewa mafunzo ya namna ya kuwakinga vijana wwnzao na viashiria hatarishi na virusi vya UKIMWI
Wataalam hao ambao watatumia afua ya michezo kufikisha elimu hiyo wameaswa kuwa mabalozi wazuri kwa mpango huo ili kuvutia wadau kuendelea kuamini zaidi katika vijana wazawa.
Wito huo umetolewa Leo 16 Mei, 2024 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa majaribio wa wataalamu wa kujitolea kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na US Peace Corps ambao utatekelezwa katika wilaya za Bahi, Chamwino na Mafinga.
Akizungumza katika hafla hiyo.Dkt. Magembe amesema wachache walio pata nafasi hiyo wakawe mabalozi wazuri wa mpango huu, kwa kuzingatia yale waliyo elekezwa ili kuvutia zadi wadau wetu kuendelea na utaratibu wa kutumia vijana wazawa
“Matarajio ya serikali ni kuona kuwa nyie ambao mmepata nafasi hii mnafanya kazi kwa bidii, uaminifu na kujitoa kwani mpango huu una faida nyingi ikiwemo ajira hasa kwa vijana pamoja na kuwajengea uzalendo na kujitoa kwa ajili ya nchi yako,” amesema Dkt. Magembe
Pia Dkt. Magembe amesema mpango huo utasaidia kuwawezesha vijana kiuchumi kama hatua moja wapo ya kuwaondoa katika viashiria hatarishi kwa kuzingatia takwimu zina onesha vijana wengi wapo katika hatari ya kupata virusi vya UKIMWI.
“Kuna mambo mengi yanayo wazunguka vijana na Kitu kimoja wapo ambacho kinasababisha vijana kuingia katika mambo hatarishi ni kutokuwa na nguvu ya kiuchumi hivyo basi katika afua tulizo nazo kuwawezesha vijana kiuchumi ni hii” ameongeza Magembe
Aidha Dkt. Magembe amewaomba wakurugenzi wa Halmashauri ambazo yanafanyika majaribio ya Mpango huo kuwapa ushirikiano mzuri vijana hao ili kuhakikisha elimu wanayo pewa wanaweza kuifikisha kwa vijana wenzao bila kikwazo”. Magembe
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Wafanyakazi wa Kujitolea la Kimarekani (Peace Corps) Bibi. Stephanie Joseph de Goes,amesema kuwa mpango huo umeshirikisha vijana kutokana na kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi.
Naye mmoja kati ya wahitimu wa mafunzo hayo Bi.Judith Maganga kutokea wilaya ya Bahi amesema wamejipanga vizuri kama vijana kuwafikia vijana wenzao walioko mitaani kuwapa elimu juu ya kujiepusha na Maambukizi ya virusi vya UKIMWI na tabia hatarishi ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya na ngono zembe.