Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, akizungumza Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema pamoja na mambo mafanikio mengine mengi, sekta hiyo imefanikiwa kuongeza Ushiriki wa Tanzania kwenye masuala ya kikanda na kimataifa kwa kwa Mwaka wa Fedha 203/24.
Waziri Nape amesema hayo wakati akielezea mafanikio mbalimbali katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024, ikiwa ni sehemu ya uwasilishaji bajeti ya wizara hiyo leo Mei 16, 2024 Bungeni jijini Dodoma.
” Tumefanikiwa kuongeza ushiriki wetu hasa kwa Mashirika kama Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU), Shirika la Mawasiliano Afrika (ATU), Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU) na pia Mheshimiwa katika Spika kipindi hicho, Shirika la Posta Tanzania, lilishinda tuzo kutokana na kuandaa, kusimamia na kutekeleza miradi inayofadhiliwa na Umoja wa Posta Duniani,” amesema Waziri Nape.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kupata obiti mpya ya setelaiti ya 160W kwa matumizi ya Satelaiti za Utangazaji na masafa mapya yatakayotumika katika kuboresha usalama wa mawasiliano ya angani na majini, na kuwezesha kupungua kwa gharama za uwekaji wa miundombinu ya mawasiliano kwenye hifadhi za barabara, ada ya awali ikipungua kutoka Dola za Marekani 1000 hadi 200 kwa Kilomita na Ada ya mwaka imepungua kutoka Dola za Marekani 1000 hadi 100 kwa Kilomita.
Waziri Nape ameeleza mafanikio mengine kuwa ni kuwezesha ujenzi na uzinduzi wa Kituo cha Mkongo wa Baharini wa 2Africa wenye uwezo wa kusukuma kiwango kikubwa cha intaneti kuanzia 17Tbps hadi 180Tbps, kuunganisha ofisi 50 za RUWASA kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kuunganisha watumiaji 12,584 na huduma za faiba mlangoni, na kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Kituo cha kuhifadhi data Zanzibar.
Amesema pia sekta imeweza Kuhakiki na kuboresha taarifa za Anwani za Makazi katika Halmashauri tano (5), nazo ni Manispaa za Morogoro, Iringa, Singida, Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Mji wa Masasi, anwani 2,308,231 (Tanzania Bara 1,937,111 na Zanzibar 371,120) zimehakikiwa kati ya anwani 12,385,956 zilizokusanywa wakati wa operesheni, huku anwani mpya 505,436 zikiwa zimesajiliwa na kufanya idadi ya Anwani za Makazi zilisosajiliwa kuongezeka hadi 12,891,392 sawa na ongezeko la asilimia 4.1.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kufanya maboresho ya mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kuwezesha kutoa barua za utambulisho wa ukaazi kupitia Watendaji wa Kata na Shehia kidijitali, moduli iliyozinduliwa Aprili 2024 kwa majaribio, na hadi sasa jumla ya barua 708 kutoka mitaa 152 zimeombwa na kutolewa.
Waziri Nape amesema pia sekta imetoa ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 20 wa Serikali katika nchi za Ujerumani, Uingereza, Malaysia na Marekani, na tayari Serikali imetangaza nafasi nyingine 480 za mafunzo ya muda mfupi kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali, na kuanza utekelezaji wa mradi wa Muundombinu wa Kitaifa wa Saini za Kielektroniki (NPKI).
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kukamilisha ujenzi wa maabara ya uidhinishaji wa vifaa vya mawasiliano ya kieletroniki (type approval laboratory), unaojumuisha maabara ya kupima mionzi inayotokana na simu za mkononi (specific absorption rate lab) na maabara ya kupima masafa ya kifaa (radio frequency lab), kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Miji Janja (Smart Cities) katika majiji ya Dodoma, Arusha na Mbeya.
Aidha, Waziri Nape amesema, katika kipindi hicho, sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, imefanikiwa kupeleka huduma ya Wi-Fi Uwanja wa Benjamin Mkapa, Viwanja vya sabasaba, Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT) Kijitonyama na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).