Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, akizungumza Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH
Katika Mwaka wa Fedha 2024/25, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inatarajia kuanza ujenzi wa Kituo cha kuhifadhi Data Dodoma na Zanzibar, pamoja na kuanzisha kituo kimoja cha Usalama wa Mawasiliano cha Taifa.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma, na Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Nape Nnauye, wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara Mei 16, 2024, na kwamba hayo ni miongoni mwa malengo 28 yaliyopangwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha.
“Serikali pia imepanga kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vyombo vya ulinzi na usalama kama Mahakama, TAKUKURU, Polisi, Magereza, JWTZ, Usalama wa Taifa), pamoja na taasisi 100 za Haki Jinai na Taasisi nyingine za Serikali,” amesema Waziri Nape.
Amesema, mambo mengine yatakayotekelezwa ni ukamilisha wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya Simu 616 ili kufikia minara 758 katika kata 713, pamoja na kuanza ujenzi wa minara mingine mipya 636 ili kuhakikisha maeneo yaliyobaki yanapata mawasiliano.
Aidha, Waziri Nape amesema, wizara imepanga kuiongezea nguvu minara 135 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G na/au 4G, kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo 70 ya kimkakati mathalan maeneo ya hifadhi na mipakani, kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye Wilaya 40 nchini, na katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika.
Ametaja mipango mingine kuwa ni kuendelea kuimarisha mifumo ya kusimamia na kupima ubora wa huduma za mawasiliano ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma na usimamizi wa sekta, kuwezesha Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kuunganishwa na mifumo mingine ya kutolea huduma za kijamii.
“Serikali inapanga kufanya ununuzi wa magari mawili maalum ya kurushia matangazo mbashara (OB Van) na magari 15 kwa ajili ya shughuli za utangazaji katika vituo vipya vya kurushia matangazo ikiwemo kuwezesha kutangaza shughuli za Uchaguzi Mkuu na wa Serikali za Mitaa,”.
Amesema Serikali pia itaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari, kuratibu uanzishaji wa Wakala wa Anga za Juu Tanzania, kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Anga za Juu na kutengeneza na kutumia mfumo wa kukusanya na kusambaza mizigo.
Aidha, Serikali kupitia Wizara hiyo, inakusudia kusimamia uundaji wa mfumo wa kidijitali utakaowezesha biashara Mtandao (e-Commerce), kutekeleza mradi wa kujenga kituo cha kikanda kitakachojumuisha maghala maalum ya kuhifadhi bidhaa, huduma ya ugomboaji na ushuru wa forodha ili kuwezesha biashara mtandao