Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TEMESA Bi.Josephine Matiro, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Mei 10,2024 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya TEMESA katika Mkoa wa Dodoma kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
……………..
KATIKA kipindi cha Miaka Mitatu ya Dodoma na Samia, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imeweza kutoa zaidi ya shilingi Bilioni 7.2 ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa karakana mpya na ukarabati.
Hayo yamesemwa leo Mei 10,2024 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TEMESA Bi.Josephine Matiro,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya TEMESA katika Mkoa wa Dodoma kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa Serikali kupitia TEMESA imeanza mchakato wa usanifu wa karakana mpya na ya kisasa ambayo itajengwa katika maeneo ya Kizota Mkoani Dodoma.
“Karakana hiyo inatarajiwa kuwa ya kisasa ambayo itaweza kuhudumia magari yote ya Taasisi za Serikali Mkoani Dodoma kwa ufanisi mkubwa. Kwa sasa iko katika hatua za usanifu chini ya mtaalamu Chuo cha Adhi.”amesema
Bi.Josephine amesema kuwa Kwa upande wa ukarabati wa karakana ya Mkoa Dodoma, mkandarasi tayari amekwishapatikana ambaye ni M/S Wagerasi Investment Ltd kutoka Dar es Salaam na mkataba umekwisha sainiwa wenye thamani ya kiasi cha Shilingi Milioni 973,747,589.96 pamoja na VAT. Mkandarasi huyo anatarajiwa kuanza kazi muda si mrefu ili kuboresha utoaji huduma katika karakana yetu ya Mkoa Dodoma.
Aidha, katika kipindi cha Miaka Mitatu ya Dodoma na Samia, Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kununua vitendea kazi vipya, karakana ya Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa karakana ambazo zimefaidika kwa kupata vitendea kazi hivyo vilivyogharimu kiasi cha shilingi Milioni 545,827,514.20 ambavyo vinaendelea kutumika na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa karakana hiyo.
Wakala pia umekuwa ukiwapeleka kwenye mafunzo wataalamu wake ikiwemo mafundi ili waweze kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea kutokea mara kwa mara kwenye magari
Aidha, ili kuendelea kuboresha huduma za karakana, mwezi Novemba, 2023, timu ya maofisa kutoka TEMESA walishiriki katika mkutano wa ushirikiano kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu sekta ya ujenzi uliofanyika hapa Dodoma ambapo TEMESA na Wakala wa karakana Kuu ya Magari Zanzibar waliingia mashirikiano katika kuwajengea uwezo mafundi kuhusu masuala ya ufundi na matengenezo ya magari.
Aidha,amesema kwa upande wa Umeme, viyoyozi, majokofu, TEHAMA na Elektroniki, Serikali pia imekuwa ikitoa vitendea kazi kila mwaka na imekuwa ikifanya hivyo ili kuhakikisha TEMESA inapata vitendea kazi vya kisasa na kuweza kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yanaendelea kujitokeza.
“Kikosi cha Umeme Kanda ya Kati Dodoma, kimefaidika kwa kupatiwa vitendea kazi kwa ajili ya kutekeleza kwa urahisi na ufanisi majukumu yake ya kila siku ya kusimika mifumo ya TEHAMA na Umeme na elektroniki katika majengo mapya ya Serikali yanayoendelea kujengwa katika mji wa Serikali Mtumba Mjini Dodoma.”amesema
Hata hivyo amesema kuwa TEMESEA imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme hapa Mkoani Dodoma ikiwemo kusanifu na kusimika mifumo ya umeme, mifumo ya TEHAMA na mifumo ya viashiria moto, mifumo ya lifti, kangavuke pamoja na mifumo ya upozaji hewa katika majengo mbalimbali yanayoendelea kujengwa katika Makao Makuu ya Nchi Dodoma.
Aidha, Wakala pia kupitia kitengo cha Huduma za Ushauri (TEMESA Consultancy Service Unit) imekuwa ikishiriki katika kufanya kazi za usanifu na kutoa ushauri wa kitaalamu na kusimamia majengo yanayoendelea kujengwa katika Mji wa Serikali (Magufuli City) ulioko Mtumba mjini Dodoma yakiwemo majengo ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Madini, Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Tume ya Madini.
Amesema kuwa wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya usimikaji wa mifumo hiyo katika majengo yanayoendelea kujengwa likiwemo jengo la Wizara ya Ujenzi ambapo usimikaji wa mifumo ya umeme mpaka sasa umefikia zaidi ya asilimia 73% pamoja na jengo la Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo usimikaji wa mifumo hiyo umefikia zaidi ya asilimia 98%.
Aidha amesema katika Miaka Mitatu ya Dodoma na Samia pia inaenda na mabadiliko ya Kiteknolojia na Wakala haujakaa mbali na suala la Teknolojia, Wakala umeweza kutekeleza na unaendelea kutekeleza miradi ya Usimikaji wa Mifumo ya Kielekroniki. Katika ofisi zake za Makao Makuu Dodoma, umesimikwa mfumo wa kufuatilia mapato yanayokusanywa katika vivuko Nchi nzima kwa kutumia mfumo wa Point of Sales) POS.
Aidha Mfumo wa kusimamia matumizi ya mafuta katika Vivuko na mfumo wa ukusanyaji mapato Kigongo-Busisi unaendelea kuboreshwa. Gharama zilzizotumika katika kusimika mifumo hiyo ni jumla ya shilingi Bilioni 5.9.
“Wakala unatekeleza miradi hiyo ya usimikaji wa mifumo ya kielektroniki kwa lengo la kuboresha Utendaji kazi wa Wakala na kuweka uwazi katika shughuli za Wakala ikiwemo suala la ukusanyaji wa mapato.”
Fedha zote zilizotumika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo ni fedha za ndani zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha amesema kuwa wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo pamoja na kuimarisha utendaji wa Wakala ikiwemo kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika eneo la ujenzi wa vivuko vipya, ujenzi wa karakana mpya na maboresho ya karakana zilizopo ili kuhakikisha TEMESA inaendelea kutoa huduma Bora kwa Fursa za Maendeleo.