NA VICTOR MASANGU,DAR
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka wa 2024 Godfrey Msava amewapongeza kwa dhati viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Pwani kwa kuweza kuwa kitu kimoja katika kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo imempelekea kuridhishwa na kuipitisha miradi 26 kati ya 28 iliyotembelewa.
Kiongozi huyo alibainisha kwamba amefurahishwa kuona ushirikiano mzuri alionao Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge pamoja na timu yake nzima ya wakuu wa Wilaya,wakurugenzi pamoja viongozi wengine kwa kuwapa ushirikiano katika kipindi chote walipokuwa katika kutembelea miradi mbali mbali.
“Tumetembelea miradi mbali mbali ya maendeleo katika Mkoa wa Pwani na nimefarijika kuona idadi kubwa tumeweza kuifungua na mingine kuiwekea mawe ya msingi lengo kubwa ni wananchi wetu waweze kupata huduma stahiki kwani Rais wetu anatoa fedha kwa ajili hiyo,”alisema Mzava.
Mzava aliyabainisha hayo leo wakati wa halfa fupi ya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru ambao ulikuwa unatokea Wilayani Mafia na kukabidhiwa rasmi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.
“Nawashukuru sana kwa dhati viongozi wote wa Mkoa wa Pwani kwa kututunza tangu siku ya kwanza hadi hii leo hatuna budi kuondoka lakini kiukweli mmefanya kazi kubwa katika miradi yenu kwa hiyo niwapongeze sana Mkuu wa Mkoa na timu yako yote,”alisema Mzava.
Pia alisema katika Mkoa wa Pwani tangu wapokelewa wameweza kupata fursa ya kutembelea,kugagua na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo imeweza kugusa katika nyanja mbali mbali.
Pia aliwaomba viongozi kuendelea kusimamia fedha ambazo zinatolewa na Rais wa awamu ya sita na katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwakumbusha kuifanyia kazi miradi ambayo imeonekana kuwa na dosari.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge akisoma taarifa kwa kiongozi huyo alibainisha kwamba mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa zimeweza kukimbizwa katika Halmashauri tisa zilizopo katika Wilaya saba za Mkoa wa Pwani.
Kunenge alibainishwa kwamba katika Mbio hizo zimeweza kupita katika miradi 28 ambayo kati ya hiyo miradi 26 ya maendeleo imeweza kupitishwa na miradi miwili haikuweza kupitishwa kutokana na kuwepo kwa baadhi ya dosari katika miradi miwili ambayo nayo itasimamiwa na kufanyiwa kazi.
Kadhalika Kunenge alifafanua kwamba miradi yote ambayo imepitiwa na mbio za Mwenge wa uhuru ina jumla ya thamani ya kiasi cha shilingi trilioni 8.5.
Pia Kunenge alimpongezs Rais wa awamu ya sita Dkt..
Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutafuta fedha mbali mbali pamoja na kushirikisha wadau kwa lengo la kuweza kuwaletea wananchi maendeleo.
Mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa ukiwa katika Mkoa wa Pwani umeweza kukagua,kuzindua,kuweka mawe ya msingi pamoja na kupitia miradi mbali mbali za maendeleo ikiwemo afya,elimu, maji,barabara,rushwa,ukimwi,madawa ya kulevya,shughuli za kimaendeleo na mambo mengine ya kijamii.