TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TANZANIA KUWA MWENYEKITI WA BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA UMOJA WA AFRIKA, MWEZI MEI 2024
Kuanzia tarehe 1 Mei 2024, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua Uenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU), ambao utadumu hadi tarehe 31 Mei 2024. Katika kipindi hicho Baraza litaadhimisha Miaka 20 tangu lilipoanza kutekeleza majukumu yake mwezi Mei 2004. Kwa msingi huo, Baraza litafanya tathmini ya mafanikio iliyopata, changamoto iliyokutana nazo na matarajio yake ya baadaye.
Aidha, katika mwezi huu wa Mei 2024, Baraza limeipa kila wiki dhima mahsusi kwa kuzingatia shughuli zake mbalimbali zilizotekelezwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Hivyo, Wiki ya Kwanza, itajihusisha na usuluhishi na majadiliano; Wiki ya Pili, itahusu Masuala ya Mahitaji ya Kibinadamu, Amani na Usalama; Wiki ya Tatu, Wanawake, Vijana na Amani na Usalama; Wiki ya Nne, dhima kuu itakuwa ulinzi kwa watoto; na Wiki ya Tano, Kusaidia Misheni za Ulinzi wa Amani.
Kilele cha Maadhimisho itakuwa tarehe 25 Mei, 2024 kwa kaulimbiu isemayo “Miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwa Chombo cha Maamuzi: Miongo miwili ijayo ya Afrika ya Amani na Usalama tunayoitaka (20 Years of the AU PSC as a Standing Decision-Making Organ: The Next 2 Decades of the Peace and Security We Want in Africa)”. Kwa kuzingatia nafasi yake ya Uenyekiti, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataongoza Sherehe za Maadhimisho pamoja na Wakuu wa Nchi
na Serikali kutoka Gambia na Uganda ambao ni wajumbe wa TROIKA ya Baraza kwa mwezi Mei 2024.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria Maadhimisho hayo ni Mheshimiwa Mohamed Ould Ghazouani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika; na Mheshimiwa Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU. Siku moja kabla ya maadhimisho hayo, PSC itakutana katika ngazi ya Mabalozi ili kuandaa Tamko la Maadhimisho hayo. Aidha, siku hiyo ya tarehe 24 Mei, 2024 Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya PSC, itaandaa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambao matokeo yake yatajumuishwa katika Tamko la Maadhimisho ya Miaka 20 ya Baraza.
Mbali na Maadhimisho, Ratiba ya Shughuli za Baraza kwa Mwezi Mei 2024 chini ya Uenyekiti wa Tanzania itahusisha Kikao cha Wazi ngazi ya Mabalozi kitakachojadili Utekelezaji wa Itifaki iliyoanzisha Baraza kitakachofanyika tarehe 15 Mei 2024; Taarifa kuhusu Mchakato wa kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini Burkina Faso, Guinea, Mali, Niger na Gabon tarehe 20 Mei 2024; Kupitia Rasimu ya Msimamo wa Pamoja wa Afrika kuelelea Mkutano wa Nne wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuzuia, Kupambana na Kutokomeza Biashara Haramu ya Silaha Ndogo Ndogo na Nyepesi (Small Arms Light Weapons).
Nafasi ya Uenyekiti wa Baraza ni jukumu kubwa; hata hivyo, kama ilivyo ada, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaahidi kushirikiana na nchi nyingine wanachama katika kutekeleza jukumu hilo ipasavyo na kwa ukamilifu ili hatimaye kuweza kukidhi matarajio ya Bara letu na wananchi wake kwa ujumla.
IMETOLEWA NA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, TAREHE 6 MEI 2024