Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu
Mussa leo tarehe 03 Mei 2024 amewaongoza Watumishi wa Wizara kutembelea Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
inayoweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi.
Akizungumza alipowasili Mamlaka ya Ngorongoro, Balozi Mussa amesema
Wafanyakazi hao waliokuwa jijini Arusha kushiriki Mkutano wa Nne wa
Baraza la Wafanyakazi wa Wizara uliofanyika tarehe 02 Mei 2024, wametumia fursa
hiyo kutembelea na kujionea kwa macho eneo hilo ambalo ni la kipekee
duniani ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii
vilivyopo Tanzania kupitia njia mbalimbali ikiwemo filamu ya Tanzania: The
Royal Tour.
Kadhalika, amesema Wizara kama mdau wa sekta ya utalii nchini imetumia mkutano
wa Baraza Kama fursa kwa kuwapa Wafanyakazi nafasi ya kufanya utalii wa ndani,
ili kujifunza na kujenga uwezo wa kutangaza kivutio hicho na vingine vingi
kikamilifu kutokana na kujionea kwa macho na kupata kwa undani taarifa muhimu
kuhusu vivutio hivyo.
“Si vyema unapomwambia mtu kuhusu kitu fulani wakati wewe mwenyewe hukijui
au hujafika, kwani tunaamini kwamba kuona ni kuamini. Hivyo tupo hapa kujifunza
na kuwafunza wengine kuhusu utalii wa ndani na tusiwaambie tu wageni kuhusu
eneo hili wakati sisi wenyewe hatulijui” amesema Balozi Mussa.
Kadhalika amepongeza
jitihada za Mhe. Rais Dkt Samia za kutangaza utalii hususan kupitia filamu ya
The Royal Tour na kusema matunda yake yameonekana kutokana na ongezeko kubwa la
idadi ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi wanaotembelea vivutio vya utalii
vilivyopo nchini.
“Filamu ya Royal Tour iliyoongozwa na Mhe. Rais Samia haikutoa matokeo kwa
watu wa nje tu bali imetoa matokeo, mvuto na ushawishi hata kwa wananchi wa
ndani wakiwemo Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki tunaunga mkono na tunatekeleza kile ambacho Mhe. Rais amekianza na
kimeleta ushawishi mkubwa kwa watu kutembelea nchini”, amesema Balozi Mussa.
Balozi Mussa ametumia wasaa huo kutoa wito kwa wananchi wa Tanzania na wageni
kutembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kujionea wanyama wakubwa watano
maarufu kama “The Big Five” wanaopatikana katika Hifadhi hiyo kama
Simba, Tembo, Chui, Nyati na Faru.
Kwa upande wake, Afisa Utalii wa Mamlaka ya Ngorongoro, Bw. Orgoo Mauyai
amesema Ngorongoro ni ya kipeee na tofauti na hifadhi nyingine duniani kutokana
na binadamu na wanyamapori kuishi pamoja na Mamlaka hiyo ni urithi wa dunia
chini ya Shirika la Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na
ameipongeza Wizara kwa kuitembelea Mamlaka hiyo.
Pia amewahimiza Wafanyakazi wa Wizara hiyo na Watanzania kwa ujumla kuendelea
kupiga kura ili Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro itetee ushindi wake wa nafasi
ya kwanza ya kuwa Kituo Kinachoongoza Kuvutia Watalii Afrika iliyoupata mwaka
2023 kwa kupiga kura kupitia Tovuti ya utalii ya www.worldtravelawards.com. Ili kuwa mshindi
wa kipengele hicho kwa mwaka 2024.
Nao Wafanyakazi wa Wizara waliopata fursa ya kushiriki ziara hiyo wameupongeza
Uongozi wa Wizara hiyo kwa kuwawezesha kutembelea hifadhi hiyo kwani
imewawezesha kufahamu mambo mengi yenye manufaa katika utekelezaji wa majukumu
yao na katika maisha yao kwa ujumla.
“Nimefurahi kuwa hapa leo. Nimejionea kwa macho uzuri wa hifadhi hii
napongeza viongozi waliofanikisha hili kwani tumejifunza mengi” alisema
Bi. Lilian Mushi.