Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MDAU wa maendeleo wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Taiko Kulunju Oletipa, amepongezwa kwa kitendo cha kununua matenki mawili ya maji ya ujazo wa lita 10,000 kwa ajili ya kutumiwa na wakazi wa kitongoji cha Oltepeleki kata ya Loiborsiret.
Mwenyekiti wa CCM Tawi la Loiborsiret Martin Noongululu amempongeza Taiko kwa hatua hiyo ya maendeleo kwani imefanikisha maendeleo kwa jamii ya eneo hilo.
“Nilijadiliana na mdau wa maendeleo Taiko baada ya kusikia changamoto ya matenki ya maji nikamwambia sema neno akaniambia nianze mimi nikasema nitatoa tenki moja la lita elfu 5 yeye akasema atatoa matenki mawili ya lita elfu 10 hivyo tumepata matenki matatu ya lita elfu 15,” amesema.
Diwani wa Kata ya Loiborsiret Mhe Ezekiel Lesenga Maridadi amempongeza na kumshukuru mdau huyo wa maendeleo kwa kuchangia huduma ya maji kupatikana kwenye kata yake.
“Ndugu yangu Taiko nakushukuru mno njoo nikushike mkono wa pongezi na shukrani kwa kusaidia jamii yetu iliyokuwa na changamoto ya maji,” amesema.
Chifu wa mkoa wa Manyara, Alais Koina amempongeza Taiko kwa kutoa msaada huo kwani umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya eneo hilo.
“Watendaji wa Serikali na viongozi kwa ujumla washikeni mikono na kuwakumbatia vijana wapenda maendeleo kama hawa ambao wanakumbuka kusaidia nyumbani,” akasema Chifu Koina.
Mkazi wa kata ya Loiborsiret, Karakai Barisha amesema Taiko amefanya jambo zuri kwani kero ya maji iliyodumu kwa muda mrefu katika kitongoji cha Oltepeleki imepatiwa majibu.
Mkazi wa kitongoji cha Oltepeleki Raphael Saitoti Siria ametoa pongezi kwa mdau wa maendeleo Taiko kwa kununua matenki hayo ya maji yanayotumiwa na watu na mifugo kwani yatamaliza changamoto ya maji eneo hilo.
“Matenki hayo matatu ya maji lita elfu 15 kwa ajili ya wananchi wa kitongoje cha Oltepeleki hatuna cha kukulipa ila Mungu pekee ndiyo atakulipa zaidi hongera sana tena sana umekuwa mtu wa kutumainiwa katika Wilaya yetu ya Simanjiro,” amesema.
Mkazi wa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani, Innocent Vitalis amesema ni kweli kabisa comrade Taiko Ole Kulunju anastahili pongezi nyingi.
“Kwanza ni mzalendo. anayependa nyumbani na anapenda maendeleo ya nyumbani, ukipiga hatua washike na wengine mkono, bila kumumunya maneno amekua akifanya hivi,” amesema Inno.
Amesema hapo wanapata somo vijana wanapofanikiwa waige mfano mzuri kutoka kwa Taiko.
“Watu wa kata ya Mirerani wanamfahamu kama Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kituo cha Afya kata ya Mirerani, ukienda kwao Loiborsiret unamkuta anavyotaka maendeleo na mambo yasonge mbele zaidi,” amesema.
Hata hivyo, Taiko amewashukuru wote waliompongeza kwa hatua hiyo na ameahidi kushirikiana na wana Simanjiro katika kufanikisha maendeleo.