Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Anne Kilango Malecela (Mb), akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Wizara ya Ujenzi wakati wa Semina kuhusu Mikakati ya Serikali ya kuongeza ushiriki wa Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi iliyofanyika jijini Dodoma.
…………….
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Wizara ya Ujenzi kusimamia kikamilifu mikakati ya kuongeza ushiriki wa Wazawa kwenye kazi za ujenzi na utekelezaji wa miradi ili kuongeza ajira na ujuzi kwa Wataalam wa ndani, kujenga Makampuni ya ndani kuwa na uwezo wa kushindana pamoja na fedha za miradi kubaki nchini na kutumika kukuza biashara za Watanzania.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Anne Kilango Malecela (Mb) jijini Dodoma Mei 04, 2024 katika Semina kwa Kamati kuhusu mikakati ya kuongeza ushiriki wa wazawa kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi ili kustawisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
“Wizara ya Ujenzi mmeanza vizuri kwa mikakati hii, Somo mlilotupa mmetusaidia kuelewa kwa kina na niwasihi msikate tamaa, simamieni hii mikakati kwa jitihada sana ili tuone mafanikio kama nchi”, amesisitiza Makamu Mwenyekiti.
Akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa mkakati wa kuongeza ushiriki wa Wazawa katika kazi za ujenzi umewasilishwa kwa Kamati ya Miundombinu ili waweze kuielewa na kutoa maoni yao ambayo yatasaidia kuhakikisha wataalamu wanakuwa wabobezi katika kazi za ujenzi na kuongeza ajira kwa watanzania.
Waziri Bashungwa ameeleza mkakati wa ushiriki wa Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi ni maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwajengea misingi imara na kusaidia Taifa kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kujenga makampuni ya ndani kuwa makubwa na uwezo wa kushindana kimataifa.
Aidha, Bashungwa ameiagiza Kamati iliyoshiriki kuandaa andiko la mikakati ya kushirikisha Wazawa kuyafanyia maboresho maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ili mkakati huo uwe bora na madhubuti.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mikakati ya kuongeza ushiriki wa Wazawa kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi, Dkt. Matiko Mturi amebainisha sababu za ushiriki mdogo wa wazawa katika miradi ya ujenzi ambazo ni pamoja na uwepo wa masharti magumu kwenye zabuni, ucheleweshaji wa malipo kwa Makandarasi na Washauri Elekezi, masharti magumu na riba kubwa ya upatikanaji wa mitaji, kutotengwa kwa miradi kwa ajili ya kukuza uwezo wa Makandarasi Wazawa, Makandarasi na Washauri Elekezi kutoa bei za chini isivyo kawaida katika zabuni.
Semina hiyo imehudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu pamoja na Viongozi na Wataalam wa Wizara wakiongozwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi,
Ludovick Nduhiye, Menejimenti ya Wizara, Watendaji na Watalaam kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akimsikiliza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Mhandisi Mwanaisha Ulenge wakati akitoa maoni kuhusu Mikakati ya Serikali ya kuongeza ushiriki wa Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika Semina iliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashunga akifafanua jambo kuhusu Mikakati ya Serikali ya kuongeza ushiriki wa Wazawa katika miradi ya ujenzi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati akifungua semina hiyo iliyofanyika jijini Dodoma
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Anne Kilango Malecela (Mb), akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Wizara ya Ujenzi wakati wa Semina kuhusu Mikakati ya Serikali ya kuongeza ushiriki wa Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi iliyofanyika jijini Dodoma
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiwa na viongozi wengine pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakifuatilia kwa karibu wasilisho la Mikakati ya Serikali ya kuongeza ushiriki wa Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wakati ikiwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati la andiko hilo Dkt. Matiko Mturi (hayupo pichani), iliyofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mikakati ya kuongeza ushiriki wa Wazawa kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi, Dkt. Matiko Mturi akiwasilisha andiko hilo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyofanyika jijini Dodoma.
PICHA NA WU