Mratibu wa Mpango wa kuimarisha familia kutoka Shirika la SOS CHILDREN’S VILLAGES Elizabeth Swai akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa jengo la Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza
Muonekano wa Jengo la Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza lililogharimu milioni 66 huku Shirika la SOS CHILDREN’S VILLAGES likiwa limechangia milioni 58
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la SOS CHILDREN’S VILLAGES linalohudumia watoto walioko kwenye hatari ya kupoteza malezi na waliopoteza malezi limechangia milioni 58 katika ujenzi wa jengo la Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza.
Jengo hilo lililogharimu zaidi ya milioni 60 lilifunguliwa jana Mei 3, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la SOS CHILDREN’S VILLAGES Florian Fanuel Mratibu wa Mpango wa kuimarisha familia Elizabeth Swai, alisema shirika hilo limechangia asilimia 83.7 ya ujenzi huo sanjari na kutoa vitanda vinne na magodoro vilivyo gharimu milioni 2.4
“Gharama za ujenzi shirika lilitoa milioni 55 baada ya ujenzi kukamilika likatoa vitanda vinne na magodoro manne ambavyo viligharimu zaidi ya milioni mbili hivyo jumla ya fedha zilizotolewa na Shiirika letu la SOS CHILDREN’S VILLAGES ni milioni 58”, alisema
Swai alieleza kuwa wanaamini kupitia uwekezaji huo watoto watapata haki zao kwani mashauri yao yatashughulikiwa kwa uhakika.
Aidha, aliiomba jamii kuendelea kufichua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto kuanzia kwenye ngazi ya familia.