*******************************
Treni ya abiria ya Deluxe yawasili Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mara ya kwanza ikitokea Dar es Salaam kwa lengo la kufanya majaribio ya njia ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali zao, hivi karibuni Desemba, 2019.
Safari hiyo ya majaribio imefanyika ikiwa ni sehemu ya utaratibu ili kuhakikisha miundombinu ya njia ya reli ni salama kwa ajili ya abiria kusafiri ambapo Maafisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini – LATRA walishiriki safari hiyo pamoja na viongozi wa Shirika la Reli wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa kuanzia Dar es Salaam hadi Moshi mkoani Kilimanjaro.
Aidha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Humphrey Polepole aliambatana na Watumishi wa TRC na LATRA katika safari hiyo ya Majaribio kuanzia Dar es Salaam – Moshi. Pia mamia ya wananchi wa mikoa ya Pwani, Tanga na Moshi wamefurahia kurejea kwa safari za treni za abiria kati ya Dar es Salaam na Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya treni ya kwanza ya majaribio kufanya safari kutoka Dar es Salaam hadi Moshi mkoani Kilimanjaro.
Wananchi hao wameonesha kufurahishwa kufuatia kurejea kwa huduma hiyo iliyosimama kwa takribani miaka 25 ambapo wananchi wa maeneo kadhaa ambayo treni hiyo ilisimama ikiwemo Wami, Mkalamo, Gendagenda, Mnyusi, Korogwe, Mombo, Makanya, Same, Kisangiro na Moshi walionekana kuishangilia treni ya Deluxe iliyokuwa ikifanya majaribio ya njia kabla ya kuanza rasmi kwa safari tarehe 6 Desemba, 2019.
Pamoja na wananchi waliojitokeza kwa shangwe kuipokea treni ya Deluxe, wapo pia viongozi wa Chama na Serikali waliojitokeza kuilaki treni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Bi. Kissa Kasongo na Diwani wa Kata ya Makanya Mhe. Damari James ni miongoni mwa viongozi waliojitokeza.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa kufanya majaribio ya njia ni suala la utaratibu kabla ya kuanza safari za treni, hivyo wananchi wakae tayari kwa ajili ya kutumia usafiri huo kwa kuwa tayari majaribio yamefanyika na ifikapo Desemba 6, 2019 safari zitaanza rasmi.
“Hili tukio tunalolifanya sasa hivi ni kwa mujibu wa sheria kutokana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini, kabla ya kuanza safari ni lazima tufanye majaribio pamoja na kutangaza nauli kwa wananchi, kwa hiyo kama nilivyosema awali safari hizi zitaanza rasmi hivi karibuni Desemba, 2019” alisema Kadogosa
Shirika linatoa rai kwa watanzania kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya reli ili kuepusha ajali na upotevu wa fedha za serikali kwa kuwa reli hii imekarabatiwa kwa fedha za watanzania, hivyo mtanzania anayehujumu miundombinu ya reli analihujumu taifa lake mwenyewe. Endapo utaona vitendo vyovyote vya kihalifu katika miundombinu ya reli tafadhali ripoti katika vyombo vya usalama au piga simu ya burem Makao makuu 0800110042 kuripoti suala hilo.