Mwenyekiti wa THBUB Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiongea katika kikao kilichofanyika Desemba 2, 2019 katika ofisi za Baraza la Wawakilishi. Kulia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Visiwani Zanzibar, Zubeir Ali Maulid.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Visiwani Zanzibar, Zubeir Ali Maulid akiongea katika kikao baina yake na Mwenyekiti wa THBUB.
Kamishna wa THBUB, Nyanda Shuli akiteta jambo na Spika wa Baraza la Wawakilishi Visiwani Zanzibar, Zubeir Ali Maulid mara baada ya kikao.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akisimama kutoa salamu za heshima alipokuwa akitambulishwa katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati kikao kinaendelea Desemba 2, 2019. Mwenyekiti alikuwa ni mgeni wa Spika.
……………….
Na Mbaraka Kambona,
Spika wa Baraza la Wawakilishi Visiwani Zanzibar, Zubeir Ali Maulid amemueleza Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu kuwa kazi aliyopewa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni kubwa na ngumu.
Spika Maulid alieleza hayo katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za Baraza la wawakilishi mapema leo (Desemba 2, 2019) alipotembelewa na Mwenyekiti huyo.
Akiongea na Mwenyekiti huyo, Spika Maulid alisema kuwa kazi ya tume sio nyepesi, kwa kuwa ni miongoni mwa vyombo vinavyotegemewa katika kuleta amani na usalama wa nchi.
“Tume ni chombo kinachotegemewa kusaidia wananchi kupata haki zao, kutoa miongozo kwa jamii namna gani wanaweza kupata haki zao”alisema Maulid
Maulid aliendelea kusema kuwa usalama na amani iliyopo nchini ni kwa sababu ya uwepo wa taasisi kama tume ambazo zinasaidia kutatua kero za wananchi.
“Hichi ni chombo cha msaada mkubwa kwa nchi, kinachoweza kuona viashiria mbalimbali vya uvunjifu wa haki za binadamu na kuweza kuishauri serikali namna nzuri ya kudhibiti kabla ya mambo kuharibika”aliongeza
Kazi hii msiichukulie kwa wepesi, ni ngumu lakini inafanyika, ipeni umuhimu mkubwa ili muweze kuishauri vizuri serikali, nina imani na wewe mwenyekiti pamoja na wenzako kuwa mnao uwezo mkubwa wa kuifanya kazi hii na kufikia malengo tarajiwa, aliendelea kusema
Aidha, Spika Maulid alimueleza Jaji Mwaimu kuwa ofisi yake ipo tayari kumpa ushirikiano wowote atakaouhitaji na pale ambapo atakuwa na ushauri wowote awaeleze nao wataupokea.
“Tupeni ushauri pale mtakapoona kuna haja ya kufanya hivyo, na sisi tutawashauri, hii sio AZAKI, ni taasisi ya serikali hivyo fanyeni kazi zenu vizuri ili muendelee kusaidia wananchi”alisisitiza
Katika ziara hiyo, Jaji Mwaimu akiongozana na viongozi wenzake wa tume, alikutana pia na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omary Othman Makungu.