Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana Dr. Bryceson Kiwelu
……………………
Hospitali ya Rufaa ya mkoa Amana imethibitisha kupokea miili miwili na majeruhi watatu wakiwa ndugu wa familia moja waliofikishwa hospitali hapo baada ya kudondokewa na ukuta wakiwa wamelala.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana Dr. Bryceson Kiwelu amethibitisha kupokea majeruhi na vifo vya watu 2.
Dr. Bryceson amesema wanafamilia hao ni wakazi wa Kipawa Jijini Dar es salaam walifikwa na madhira hayo wakiwa usingizini baada ya nyumba yao kuangukiwa na ukuta wa nyumba ya jirani yao.
Amewataja waliofariki kuwa ni Mama wa familia hiyo aliyejulikana kwa jina la Khadija Ramadhani mwenye umri wa miaka 43 na mtoto wake wa kiume Charlos Immanuel mwenye umri wa miaka 17 ambapo majeruhi wengine wa ajali hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zimeimarika.
“Tunawashukuru viongozi wa jeshi la polisi,majirani na viongozi wa serikali ya mtaa kwa ushirikiano kwa kuwezesha kuwafikisha majeruhi hao katika hospitali yetu ya amana”Ameongeza
“Pia tunawapongeza watumishi wa idara ya dharura ya hospitali kwa kutoa huduma sahihi na kwa wakati kwa majeruhi wa tukio hilo pamoja na wateja wengine”,Amesema Dr. Bryceson.