Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akijibu
hoja mbalimbali za Wabunge kabla ya Bunge la Tanzania kupitisha Bajeti
ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/2025.
…………………….
95.28% kuelekezwa kwenye maendeleo
Serikali kuja na Kanuni ya Uwajibikaji kwa wananchi Miradi ya Mafuta
na Gesi Asilia
Dkt. Biteko aagiza Halmashauri kupeleka fedha za Ushuru wa Huduma vijijini
Masharti ufunguzi wa vituo vya CNG yarekebishwa kuvutia uwekezaji
Kapinga atilia mkazo utekelezaji Nishati Safi ya Kupikia na CNG
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha shilingi
Trilioni 1.8 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati katika mwaka
wa fedha 2024/2025 ambapo asilimia 95 ya bajeti hiyo imeelekezwa
kwenye miradi ya maendeleo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akijibu
hoja mbalimbali za Wabunge ameeleza kuwa, ili wananchi wanaozunguka
miradi ya Gesi Asilia na Mafuta wafaidike na rasilimali hiyo Serikali
itapitisha kanuni itakayoongoza Miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa
Jamii (CSR) ili kampuni ziweze kuwajibika ipasavyo kwa jamii.
Aidha, kuhusu ushuru wa huduma (service levy) unaotolewa na kampuni za
Mafuta na Gesi kwa Halmashauri mbalimbali nchini, Dkt. Biteko ameagiza
Halmashauri hizo zihakikishe kuwa sehemu ya fedha hizo zinarudi kwenye
vijiji ambapo miradi inatekelezwa.
“Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI
ili kuja na mpango wa utekelezaji wa service levy ili fedha
zinazotolewa ziende pia kwenye maeneo ambapo miradi inatekelezwa, Rais
ameshaeleza hataki kuona malalamiko sehemu ambapo Gesi inachimbwa,
Service Levy na CSR sasa zitaanza kufanyiwa kazi kwa kasi kubwa.”
Amesema Dkt. Biteko
Amesisitiza kuwa, suala la CSR si siri bali ni kitu cha wazi kwa
wananchi na Wabunge hivyo ni haki kwa wananchi hao kupata taarifa za
uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na kusisitiza kampuni za kitanzania
kupewa kipaumbele kwenye miradi ili wananchi wanufaike na rasilimali
zilizopo nchini.
Kuhusu hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara miezi kadhaa nyuma,
amesema ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na upungufu wa umeme wa megawati
410 lakini sasa uwezo wa kuzalisha umeme umekuwa mkubwa kuliko
mahitaji huku mitambo minne ya Kinyerezi ikizimwa na kusubiri
changamoto itakayojitokeza.
Amesema kwa sasa kukatika kwa umeme kunaweza kutokea si sababu ya
upungufu wa umeme bali baadhi ya miundombinu ya umeme kuchoka kutokana
na kuwa ya muda mrefu pia uhujumu wa miundombinu akitolea mfano wizi
wa transfoma takribani 87 na nyaya za umeme pamoja na mvua zilizozidi
kipimo ambapo mpaka sasa nguzo 651 na transfoma 36 zimeondolewa na
maji.
Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea na maboresho ya miundombinu ya
umeme pamoja na uwekezaji kwenye miundombinu hiyo ikiwemo ujenzi wa
vituo vya kupoza umeme.
Kwa wakandarasi wanaosuasua katika kutekeleza miradi ya umeme nchini
ikiwemo kampuni za Serikali kama vile ya ETDCO, Dkt. Biteko amesema
watachukuliwa hatua kali ikiwemo za kutowapa tena miradi mingine ya
umeme.
Akizungumzia usambazaji umeme vijijini, amesema suala linalotiliwa
mkazo na Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji kwanza, kisha
vitongoji na baadaye kwenye nyumba na kwamba suala la kuwaunganishia
umeme wananchi ni endelevu.
Kwa mikoa iliyo nje ya gridi kama vile Kagera, Katavi, Lindi na Mtwara
ameeleza kuwa mikoa hiyo itaunganishwa na gridi kupitia miradi
mbalimbali inayoendelea na hii inajumuisha miradi ya kusafirisha umeme
kwenda nchi nyingine za Afrika kama vile Kenya na Uganda.
Kuhusu bei ya umeme kwenye maeneo yanayojulikana kama Vijiji-Miji (Sh.
320,000) amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo la
kuyatambua maeneo hayo na uchambuzi umeshafanyika huku maeneo 1,570
yakipatikana hivyo suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali ambapo
utaratibu wa malipo kwenye maeneo hayo utaelezwa.
Akizungumzis uanzishaji wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG),
Dkt. Biteko amesema suala hilo linachukuliwa kwa uzito mkubwa na
sasa masharti ya kuanzisha vituo hivyo yamepunguzwa ambapo wawekezaji
wakikamilisha nyaraka zinazohitajika ndani ya Siku Tatu watakuwa
wamepata leseni.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga
amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye
Sekta ya Nishati kupitia miradi mbalimbali kielelezo na maendeleo
inayoendelea nchini.
Akizungumzia Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Kapinga amesema kuwa, ni
nyenzo muhimu ya kusaidia kutunza mazingira na kwamba mkakati wa
kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia umeshapitishwa na Baraza la
Mawaziri na upo tayari kufanyiwa kazi.
Amesema azma ya Serikali ni kuongeza kasi ya matumizi ya Nishati Safi
ya Kupikia ikiwemo gesi ambapo mkakati una lengo la kuhakikisha
kunakuwa na upatikanaji wa nishati safi, salama, endelevu, yenye
uhakika pamoja na kuondoa matumizi ya kuni na mkaa kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge.
Kuhusu gharama za mitungi ya Gesi amesema suala hilo limeanza
kufanyiwa kazi na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
ambao umeanza kutoa ruzuku ya mitungi na mpaka sasa wameshatoa
mitungi 83,500 na mingine 450,000 itatolewa kwa wananchi.
Aidha, kuhusu suala la kuwa na mitungi ya kilo chache ili wananchi
waipate kwa gharama ndogo amesema tayari mitungi ya kilo tatu imeanza
kuingia sokoni na Serikali inaendelea kusimamia ili kuwa na Mawakala
wengi zaidi wa kusambaza gesi hata katika maeneo yaliyo mbali.
Vilevile kuhusu ujenzi wa vituo CNG na vya kubadilsha mifumo ya magari
ili kutumia gesi amesema kuwa tayari ujenzi wa kituo mama umeanza
katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam, vituo viwili vingine vinajengwa
katika eneo la Kairuki na Muhimbili na vingine 20 vitajengwa kwa
kushirikiana na Sekta binafsi.
Bajeti ya Wizara ya Nishati iliyoidhinishwa na Bunge ni shilingi
1,883,759,455,000 ambapo Shilingi 1,794,866,832,000 sawa na asilimia
95.28 ya Bajeti yote ya Wizara ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na
Shilingi 88,892,623,000 sawa na asilimia 4.72 ni kwa ajili ya Matumizi
ya Kawaida.