Na Ibrahim Dunia. Maelezo.
Zaidi ya vitu vyenye thamani ya Sh. Billioni 15 vimetaifishwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar (ZDCEA) baada ya kubainika kutokana na dawa za kulevya.
Akizungumza na Waandishi wa habari huko ofisini kwake Migombani wilaya ya Mjini, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Kanal Burhan Zubeir Nassoro amesema watuhumiwa wamebainika kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya katika nchi mbalimbali ikiwemo Zanzibar, Tanzania Bara, Afrika, Asia, Ulaya na Marekani.
Amesema watuhumiwa wamejipatia fedha sh. Bilioni 15 na kuzitumia kwa njia ya utakatishaji wa fedha haramu kwa kununua magari ya kifahari, nyumba, viwanja na kuanzisha biashara hewa.
‘‘Wahalifu wa aina hii wanatumia nguvu ya fedha na mbinu mbalimbali ili wasitambulike na waonekane watu wema katika jamii kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo ujenzi na ukarabati wa nyumba za ibada, kuchimba visima vya maji, kufadhili mchezo wa mpira wa miguu na kuhudumia watoto yatima’’alisema Kanal Burhan.
Aidha amesema Serikali ya awamu ya nane chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imedhamiria kwa dhati kudhibiti na kupambana na uhalifu wa dawa za kulevya Zanzibar bila kuangalia jina na wadhifa wa mtu.
Mbali na hayo amewataka watuhumiwa wanajishughulisha na biashara za haramu kujisalimisha katika vyombo vya usalama sambamba na kuwataka wananchi kutoa taarifa za watuhumiwa kama hao wakati wanapowabaini katika jamii ili kuweza kuondosha tatizo hilo.
Vitu vilivyotaifishwa ni pamoja na Gari 6, zenye thamani ya millioni 300.9, Vyombo vya usafiri majini 3, vyenye thamani ya million 200.9, viwanja na makaazi ya biashara 8, zenye thamani Billioni 6.8, Nyumba za kifahari (Beach Villa) 2, zikiwa na thamani Billioni 6.3, nyumba za makaazi na Biashara 8, zikiwa na thamani Billion 1.7 ambapo watuhumiwa wanadaiwa kutoroka nje ya nchi.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanal Burhan Zubeir Nassoro kuhusiana na Kutaifisha Mali za Watuhumiwa wa Dawa za Kulevya ambao wamekataa Wito na Kukimbia Nchini hafla iliofanyika katika Ofisi ya Mamlaka hio Migombani Wilaya ya Mjini Zanzibar.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanal Burhan Zubeir Nassoro akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Kutaifisha Mali za Watuhumiwa wa Dawa za Kulevya ambao wamekataa Wito na Kukimbia Nchini hafla iliofanyika katika Ofisi ya Mamlaka hio Migombani Wilaya ya Mjini Zanzibar.
Muandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi Jesse Mbezi Mikofu akiuliza maswali katika Mkutano wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanal Burhan Zubeir Nassoro akizungumza kuhusiana na Kutaifisha Mali za Watuhumiwa wa Dawa za Kulevya ambao wamekataa Wito na Kukimbia Nchini hafla iliofanyika katika Ofisi ya Mamlaka hio Migombani Wilaya ya Mjini Zanzibar.