Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Viongozi na Watanzania wanajifunza mengi kutokana na historia ya utendaji kazi wa Mzee John Samwel Malecela katika nyadhifa mbalimbali alizoshika Serikalini na Chama cha Mapinduzi na ataendelea kuwa hazina muhimu ya maarifa na uzalendo hapa nchini.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika sherehe za Kumbukizi ya miaka 90 ya kuzaliwa Mhe.Mzee John Samwel Malecela, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nyumbani kwake Uzunguni Jijini Dodoma tarehe:21 Aprili 2024.
Aidha Rais Dk.Mwinyi amempongeza Mzee John Samwel Malecela kwa kutimiza umri huo na amemuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia umri mrefu na afya njema.
Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Watanzania wataendelea kufaidika na busara, hekima, na ushauri wake katika kuiletea maendeleo nchi yetu na uzoefu wake mkubwa alionao Mzee Malecela katika uongozi, siasa na diplomasia ya Kimataifa.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama cha
Mapinduzi na Dini Wamehudhuria akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.Cleopa Msuya, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Comrade Abdulrahman Kinana, Spika wa Bunge Mstaafu Mhe.Job Ndugai, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule, Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Mary Chatanda.