Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe, Dkt. Doto Biteko akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha Afya Shehiya ya Kinyikani Jimbo la Kojan wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba tarehe 20 Aprili 2024. Wa kwanza kulia (mbele) ni Mbunge wa Jimbo la Kojani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hamad Chande
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe, Dkt. Doto Biteko,akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha Afya Shehiya ya Kinyikani Jimbo la Kojan wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba tarehe 20 Aprili 2024.
………….
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka Watanzania katu wasikubali kugawanywa kwa namna yoyote na badala yake waulinde na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao unatimiza miaka 60 ifikapo tarehe 26 Aprili, 2024 na serehe za maadhimisho yake yatafanyika Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Biteko amesema kuimarika kwa Muungano kumetokana na Amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa Watanzania na hivyo Muungano ni moja ya Tunu za Taifa ambao unahitaji kulindwa ili kuenzi matunda yaliyopatikana.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo 20 Aprili 2024, mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Shehiya ya Kinyikani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho kuelekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Tanzania ndio nchi pekee barani Afrika na Duniani kwa ujumla kuwa na Muungano imara na thabiti kwa miaka mingi, hivyo ni vema kuulinda kwa namna yoyote ile” Alisema Dkt. Biteko
Awali, Dkt. Biteko alipata fursa ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha Afya cha Kinyikani, kinachojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) na kusimamiwa na wakala wa ujenzi Zanzibar ZBA, ambapo hadi kukamilika kwake kituo hicho kitagharimu shilingi milioni 500.
Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo zikiwemo Zahanati, Vituo vya Afya, Shule na Miundombinu mbalimbali inatekelezwa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa nchi Afisi ya makamu wa pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma, amepongeza jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwaletea wananchi maendeleo na kuhakikisha huduma za Afya zinaimarika kisiwani Pemba.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kojani Mhe. Hamad Chande, amewashukuru wananchi wa Jimbo la Kojani kwa kuchangia Takriban asilimia 10 ya ujenzi wa kituo hicho cha Afya
pamoja na nguvu kazi kwenye ujenzi wa kituo hicho, na kuwaahidi pindi ujenzi utakapokamilika atatoa gari la jipya la wagonjwa ili kurahisha huduma kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kituo hicho cha afya kitakuwa na huduma mbalimbali ikiwemo huduma za wagonjwa wa Nje OPD, Huduma za Uzazi Mama na Mtoto, Huduma za Maabara, Ultra Sound, Pamoja na huduma nyingine za tiba.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa nchi Afisi ya Makamu wa pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma, pamoja na viongozi wengine na wawakilishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASA, Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatafikia kilele chake tarehe 26 Aprili, 2024 katika sherehe za Kitaifa zitakazofanyika Jijini Dar Es Salaam.