Na Magreth Kinabo – Mahakama, Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) kutumia silaha ya elimu ya sheria kuitumikia jamii kikamilifu.
Aidha, Jaji Mkuu amesema kwamba wahitimu hao wanapaswa kuinoa elimu hiyo kila wakati ili silaha hiyo iwe na nguvu ya kuibadilisha dunia.
Prof. Juma alisema hayo katika sherehe za mahafali ya 19 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa wahitimu wa Stashada na Astashahada ya Sheria, yaliyofanyika leo Novemba 29, mwaka huu chuoni hapo, wilayani Lushoto mkoani Tanga.
‘Katika fani ya sheria, moja ya njia ya kuinoa silaha hiyo ni kujisomea kila wakati kwa sababu sheria na kanuni huwa zinabadilika mara kwa mara. Sio vyeti vyenu vitakavyofanya kazi ya kutoa huduma. Kwa kuhitimu hivi leo haina maana kwamba mtakuwa mmemaliza kujifunza masuala yote ya kisheria.
‘Bali mnapaswa kuendelea kuwa wanafunzi kila wakati ili kujua sheria mpya na kanuni zake pindi zinapobadilika. Mhitimu mzuri ni yule anayeacha milango wazi ya kujifunza kutoka kwa wengine’.alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu aliwaasa wahitimu hao, popote pale watakapokuwa kujifunza jambo jipya kila siku ili wasipitwe na wakati ili kutoiaibisha fani yao, hivyo wajiendeleze hadi kufikia viwango vya juu kabisa katika fani hiyo muhimu.
‘Jengeni tabia ya kujisomea wenyewe vitabu ili kuendelea kujielimisha. Kamwe usimtegemee mtu mwingine asome kisha akuelekeze. Katika kujisomea, hakikisheni mnasoma pia mambo yasiyo ya kisheria kwa mfano hivi karibuni, Mhe. Benjamin William Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu) alizindua kitabu chake “My Life” My Purpose, A TANZANIA PRESIDENT REMBERS”,’ alisisitiza.
Alisema kitabu hicho kitawaongezea ufahamu wa historia ya nchi yetu kupitia miaka 81 ya maisha ya Rais huyo wa Awamu ya Tatu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho, lililomaliza muda wake, Mhe.Jaji Dkt. Gerald Ndika, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema mahafali haya ya 19, yamefanya jumla ya wahitimu 6,037 katika ngazi ya Stashahada na Astashada ya Sheria tangu kilipoanzishwa mwaka 2001.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Mhe Jaji Dkt.Paul Kihwelo alizitaja takwimu za wahitimu hao kwa mwaka huu, kwa upande wa Stashahada ya Sheria kati ya wahitimu 169 wanaume ni 93 (55.03%) na wanawake 76 (44.97%) na kwa upande wa Astashahada ya Sheria, kati ya wahitimu 234 wanaume ni 102 (43.59%) na wanawake ni 132 (56.41%).
Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, pia baadhi wahitimu walizawadiwa vyetieti, vitabu pamoja na fedha taslimu kutoka chuo hicho na Mahakama yaTanzania.
Pia wahitimu bora wawili kutoka kutoka ngazi hizo, waliopata wastani wa daraja ‘A’ katika somo la mwenendo wa mashauri ya madai na jinai walipewa zawadi kutoka kwa Jaji Mkuu.