Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ujenzi wa Chuo cha mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera mkoani Kagera.
Balozi wa China nchini Tanzania WANG Ke akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma Cha Mkoa wa Kagera.
Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo cha ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi waliohudhuria uzinduzi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Kagera wakifuatilia hotuba ya waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua kuanza kwa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha mkoa wa Kagera, mkoani Kagera.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akishikana mkono na Balozi wa China nchini Tanzania mara baada ya uzinduzi wa ujenzi wa Chuo cha VETA cha mkoa wa Kagera.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Balozi wa China nchini Tanzania WANG Ke pamoja na viongozi wengine wa mkoa wa Kagera wakiweka udongo kwenye mti ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Chuo cha VETA cha mkoa wa Kagera.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwasili katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Chuo cha VETA cha mkoa wa Kagera.
…………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera na kusema kuwa ujenzi wa chuo hicho ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kunakuwa na Vyuo vya ufundi stadi vya Mikoa na Wilaya.
Akizindua ujenzi wa chuo hicho mkoani Kagera Waziri Ndalichako amesema chuo hicho kinajengwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kutokana na uhusiano mzuri wa muda mrefu tulio nao na kwamba pindi ujenzi utakapokamilika vijana wengi wa kitanzania watapata fursa ya kusoma katika chuo hicho na kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazo fundishwa.
“Kama nilivyosema Tanzania na China ni marafiki na rafiki yako anaangalia mahitaji yako, waswahili husema akufaaye kwa dhiki ndio rafiki wa kweli. China imeona Tanzania inajenga uchumi wa Viwanda ikiwa ni azma ya serikali ya awamu ya Tano nao wakaamua watuunge mkono katika ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi ili kuandaa vijana wenye ujuzi watakaofanya kazi katika viwanda.
“Nikuombe Balozi tufikishie shukrani zetu za dhati kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa msaada huu mkubwa na wa kihistoria ,”aliongeza Waziri Ndalichako
Waziri Ndalichako amesema ujio wa mradi huo utaongeza ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwa wazawa 400 wataajiriwa katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kupata ujuzi kulingana na kazi watakazokuwa wakizitekeleza.
“Vijana watakaofanya kazi eneo la mradi pamoja na kufanya kazi watapata na mafunzo, kwa hiyo ujuzi wao wa kiufundi utaimarishwa kupitia kazi ambazo watakuwa wakifanya katika mradi,”alisema waziri Ndalichako.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kupitia upya fani zilizopangwa kutolewa katika chuo hicho ili ziendane na Mazingira halisi ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.
“Nimepitia fani ambazo zimeanishwa kutolewa katika chuo hiki pindi kitakapokamilika, nikiangalia eneo ambalo chuo kinajengwa ni eneo la ziwa na watu wa Kagera au wazazi wa hapa ni wavuvi lakini sijaona kozi ya uvuvi sasa tunawaletea mambo ya uchomeleaji, ufundi bomba, useremala, upakaji rangi kwenye bahari, nilitegemea kuwe na fani ya uvuvi pia
tuweke fani zinazoendana na mazingira,” alisema Waziri Ndalichako
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Balozi WANG Ke amesema Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania amezingatia maboresho ya sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwaongoza watanzania kuelekea dira ya maendeleo 2025 hivyo China iko tayari kuchangia maendeleo katika sekta ya elimu ili kufikia malengo ya elimu ambayo serikali ya tanzania imejiwekea.
Nae Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti amewataka wanakagera hasa vijana kushiriki vizuri katika kazi za ujenzi zitakazofanyika katika mradi huo ili kupata ujuzi wa ufundi ambao utawasaidia kushirikia katika kazi za ujenzi zitakazojitokeza katika Mkoa wa Kagera mara baada ya mradi kukamilika.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema Chuo hicho kinajengwa katika eneo lililotolewa na wananchi wa kijiji cha Burugo wilayani Bukoba na lina ukubwa wa hekta 40. 5 sawa na hekari 100.
Dkt. Bujulu amesema Chuo hicho pindi kitakapokamilika kitatoa fani za useremala, uchomeleaji, upakaji rangi, ufundi bomba na kitachukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2000 wa kozi fupi
Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera kinajengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama za fedha za kitanzania sh bilioni 19.4 ambapo ujenzi wake utachukua miezi 18
Gharama hizo zinajumuisha usanifu, upembuzi yakinifu na ujenzi mpaka ukamilike.