Kaimu Katibu Msaidizi ,Ofisi ya Rais , Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma Selemani Sabihi Chihembe akiangalia usaili kwa njia ya mfumo “ONLINE APTITUDE TEST” wakati ulipozinduliwa huko Taasisi ya Karume (KIST) Mbweni Zanzibar.
Baadhi ya vijana wakiwa katika usaili kwa njia ya mfumo “ONLINE APTITUDE TEST” uliozinduliwa kwaajili ya kurahisisha zoezi hilo,hafla iliyofanyika Taasisi ya Karume (KIST) Mbweni Zanzibar.
Afisa ICT Chuo cha Karume Zanzibar Omar akisimamia zoezi la usaili kwa njia ya mfumo “ONLINE APTITUDE TEST” wakati ulipozinduliwa huko Chuo cha Taasisi ya Karume (KIST) Mbweni Zanzibar.
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Rahma Khamis. Maelezo.
Vijana wanaoomba nafasi za ajira wametakiwa kufanya usajili kupitia mfumo wa kuandika kidigitali (ONLINE APTTUDE TEST) ili kurahisisha usajili na kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza mara baada ya kuzindua mfumo huo Kaimu Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Secretary ya Ajira katika Utumishi wa Umma Suleiman Sabihi Chichembe huko katika Chuo Cha Ufundi Karume (KIST) Chukwani Wilaya ya Magharibi ‘B’ amesema mfumo huo utaondosha usumbufu kwa Wasaili na Wailiwa.
Aidha amefahamisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza kufuata masafa ya mbali kufanya usaili kwa waombaji hao na kuweza kufanya popote walipo jambo ambalo litapunguza uchelewaji wa kufika sehemu husika pamoja na gharama za usafiri.
Ameongeza kuwa kuna baadhi ya maeneo yanakuwa na changamoto ikiwemo usafiri jambo linalochangia kutokufika kwa wakati na kupelekea kukosa kufanya usaili huo.
Amefahamisha kuwa uzinduzi huo kwa hatua ya mwazo wameanza na Maafisa Tehama kupitia kada mbalimbali ikiwemo watu wa programu, data base pamoja na Security na wanajiandaa kwenda katika kada nyengine.
“Tuna mpango mkakati wa kutoa taarifa na kutembelea vyuo vya kati, juu na elimu ya sekondari ili wapate elimu na kujuwa kutumia mfumo huu.” alisema Msaidizi huyo.
Akizungumzia kuhusu mfumo huo kuunganisha katika sehemu zinazohusiana na utoaji wa ajira amesema tayari mfumo huo umeshaunganishwa katika taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Katiba na Sheria, Tume ya Utumishi Serikalini, Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na maeneo mengine.
Hata hivyo amewataka vijana kuendelea kuomba nafasi na kufanya usaili kupitia mfumo huo na kutembelea tovuti ya Zan ajira na Ajira Portal ili kuweza kuona nafasi zilizotangazwa na endapo kutajitokeza changamoto yeyote kuweza kutoa taarifa.
Nae Afisa Msimamizi ICT Karume Omar amesema mfumo huo utaondoa changamoto zilizopo kwani unatoa maelekezo namna ya matumizi ukilinganisha na zamani ambapo ilikuwa lazima wawepo wasimamizi.
Nao Vijana waliofanya usaili kupitia mfumo wamesema mfumo ni mzuri na unarahisisha watu kuweza kufahamu kama unaendelea hatua nyengine au umekosa.
Aidha wameshauri vijana kusoma fani ya computer Science kwa vile dunia imebadilika na kupelekea kila kitu kufanya kwa kutumia mifumo.
Uzinduzi wa mfumo wa ONLINE APTTUDE TEST umezinduliwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwemo Dar-es-salaam, Pemba na Unguja.