KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt.Bashiru Ally Kakurwa, akiwahutubia Wana CCM katika uzinduzi wa kampeni ya Magharibi ya Kijani iliyozinduliwa katika ukumbi wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Bububu Zanzibar.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt.Bashiru Ally Kakurwa,akitembelea vikundi vya wajasiriamali walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Magharibi ya Kijani Zanzibar.
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Magharibi kichama ndugu Mohamed Rajab Soud, akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa kampeni ya magharib ya kijani iliyofanyika Bububu Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Zanzibar.
…………………..
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally Kakurwa, ameyaonya mashirika ya kimataifa yanayowakilisha nchi zao Tanzania kuacha kuingilia siasa za ndani ya nchi.
Alisema kuna baadhi ya wawakilishi wa nchi hizo za kigeni wameanza kutoa kauli zisizofaa na vipeperushi kupitia nchi za mitandao wakibeza na kuhoji kuhusu Uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni.
Hayo aliyasema wakati akizindua kampeni ya Magharibi ya kijani huko katika ukumbi wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Zanzibar.
Alisema ajenda ya uchaguzi huo tayari imefungwa na chama cha mapinduzi kimeibua mshindi kwa asilimia zaidi ya 99 na kwa sasa kinajipanga na Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.
Alisema watu hao wanaojadili uchaguzi katika mitadao ya kijamii ni kupoteza muda kwani mitandao haipigi kura wala kubadilisha uhalisia wa ushindi wa CCM.
“Naendelea kuwakumbusha hawa wenzetu wanaojadili uchaguzi katika mitandao kuwa Whatsapp na Instagram na facebook hazipigi kura na hazijasajiliwa katika daftari la kudumu la wapiga kura”, amesema Dkt.Bashiru.
Katika maelezo yake Dkt.Bashiru alisema kuna baadhi ya watu wanadhani demokrasia ipo katika uchaguzi tu jambo ambalo sio sahihi kwani hata kutokuwa na tama ya kukandamiza uhuru wa wengine pia ni demokrasia.
Akizungumzia kampeni hiyo iliyozinduliwa alisema kampeni ya kijani iliyoasisiwa na UVCCM imesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha shughuli za kisiasa ndani ya Chama na Jumuiya zake.
Alisema kampeni hiyo ya Magharibi ya kijani inatakiwa kutoa matokea chanya yanayoendana na malengo yaliyokusudiwa na kuimarisha shughuli za kisiasa chama ndani ya mkoa huo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Alieleza kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964 ndio yaliyofanikisha nchi kujitawala na kufikia maendeleo endelevu yaliyopo hivi sasa.
Akizungumzia Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020,alisema imetekelezwa kwa ufanisi mijini na vijiji wanapata huduma bora za kijami,kiuuchumi na kimaendeleo bila ubaguzi.
Dkt.Bashiru, alihoji wanaobeza uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein ambaye anamaliza muda wake mwaka ujao akiwa na historia nzuri na iliyotukuka ya uchapakazi na uadilifu.
Alisema Dk.Shein ni kingozi mwenye uzoefu na uwezo mkubwa kiuongozi kwani amehudumu kwa muda mrefu ndani ya ngazi za juu za Chama na Serikali.
Alisema Rais ajaye wa Zanzibar anatakiwa kuwa na sifa kama za Rais wa sasa Dk.Ali Mohamed Shein ambaye ni muadilifu,mpole na mchapakazi.
“ Nawashangaa baadhi ya wanasiasa eti wanatathimini Dk.Shein na Serikali anayoiongoza nawambia kuwa Rais huyu ni wa kuigwa kwani mambo ya maendeleo aliyoyafanya Zanzibar yanaonekana kwa kila mtu”, alieleza na kuongeza kuwa Rais huyo hadi hivi sasa hana kashifa za rushwa wala ufisadi.
Pamoja na hayo Dkt.Bashiru, aliwasihi Wana CCM kuendelea kushikamana na kulinda uhuru ulioasisiwa na Waasisi wa Chama hicho kwa gharama yoyote bila hofu.
Katibu huyo alisema ushindi uliopatikana katika uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania bara ni sehemu ya kutesti mitambo na kwa sasa anatumia ziara yake kuendelea kufunga mitambo katika Mikoa yote ya Zanzibar ili 2020 CCM ipate ushindi wa kihistoria.
Aliahidi kwamba akiwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ndani ya CCM kwa Tanzania nzima atahakikisha CCM inashinda Zanzibar na Tanzania bara katika uchaguzi mkuu ujao.
Naye Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mwl.Kombo Hassan Juma, alisema CCM inaimarika kisiasa kutokana na Serikali kutekeza vizuri Ilani ya CCM .
Mapema akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharib ndugu Mohamed Rajab Soud,alisema kampeni hiyo imezinduliwa kwa lengo la kusafisha njia ya kisiasa kuelekea 2020.