SHIRIKA la Grumeti Fund kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii katika kujenga jamii yenye usawa na yenye kujitambua kwa vijana wa kike na kiume imewakusanya pamoja wanafunzi wa kike zaidi ya 1,243 na wavulana 565 katika nyakati tofauti kutoka shule za sekondari Makundusi na Natta zilizopo wilayani Serengeti kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali za kijinsia zinazowakabili watoto wa kike na kiume pamoja na utatuzi wa changamoto hizo.
Katika kongamano la wasichana lililofanyika katika shule ya Sekondari Natta iliopo Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumeti Fund Bi. Frida Mollel amewataka wasichana kujitambua na kujua thamani yao sambamba na kutokata tamaa kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili bali watumia elimu wanayoipata ili iweze kuleta tija na mabadiliko chanya katika jamii.
“Kama unatoka katika jamii ambayo inakwambia wewe huwezi wala hufiki mbali, Grumeti Fund tumekuja kukwambia Leo kwamba unaweza kuwa yeyote unayetaka katika dunia hii kama ukijitambua, tuko hapa kuwatia moyo, tuko hapa kuwambia kuwa nyie ni taifa kubwa” alisema Bi. Frida Mollel.
Aidha, Frida Mollel aliendelea kusisitiza kuwa elimu ndio dira na njia ya kufikia ndoto za vijana hao kama watatumia nafasi waliyopewa vema watakuwa baraka katika jamii yao na katika nchi kwa ujumla.
Katika kongamano hilo shirika la Grumeti Fund imetoa msaada wa taulo za kike zinazoweza kutumika kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu (reusable pads) kwa wanafunzi wa kike 1,243 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 16,159,000 katika shule za sekondari Natta na Makundusi.
Aidha, kwa upande wake Bi. Sophia Mnandi- mratibu wa ushauri kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) katika kongamano hilo amewataka wasichana kupaza sauti zao katika kutokomeza mila na desturi kandamizi ndani ya Jamii sambamba na kuwa wavumilivu katika changamoto wanazopitia.
“Tumia muda wako kujilinda kila sehemu utakapokuwa dhidi ya Mila na desturi kandamizi ndani ya Jamii zetu, pia tumesema wewe mwenyewe ujitambue unataka kuwa nani na kwa wakati gani, hayo yote yanaitaji muda na uvumilivu” alisema Bi. Sophia
kwa upande wake mkufunzi kutoka chuo cha Afya Kisare Mwl. Restuda Murutta amewaasa wanafunzi hao kuzingatia elimu ya afya ya uzazi sambamba na kuepuka matumizi ya dawa za kupunguza maumivu wakati wa hedhi bila ushauri wa kitabibu.
“Uwapo katika siku za hedhi, ni vizuri kuzingatia usafi hasa kuosha via vya uzazi, pia usikimbilie kutumia dawa za kupunguza maumivu wakati wa hedhi bila ushauri wa daktari kwa kufanya hivyo ni kuhatarisha afya yako ya uzazi” alisema Bi. Restuda
Nao miongoni mwa wanafunzi waliopata mafunzo hayo ameishukuru kampuni ya Grumeti Fund kwa namna wanavyowajali na kuwathamini mabinti na kuahidi kuyaweka katika vitendo mafunzo hayo na kusambaza elimu kwa wengine.
Awali kongamano hili lilitanguliwa na kongamano la vijana wa kiume takribani 565 kutoka shule za Sekondari Natta na Makundusi ambapo Bi. Frida Mollel ambaye ni mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii kutoka Grumeti Fund akaweka wazi lengo la kuwakutanisha pamoja vijana wa kiume kuwa ni kutambua changamoto wanazopitia na kujaribu kutafuta majibu ya changamoto hizo kwa pamoja sambamba na kuwashirikisha wanaume katika utatuzi wa changamoto za mtoto wa kike ili wote kwa pamoja waweze kusimamamia ndoto zao. Aliwaasa vijana kutokuiga tabia na tamaduni za kigeni zinazoweza kuharibu kabisa dhamani yao na maisha yao kwa ujumla. Wafanye bidii kwenye masomo yao na kuepuka makundi rika.
Naye aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo Ndg. Wandele Rwakatare ambaye ni Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Bunda akawataka vijana wa kiume kuuvaa uhalisia wa jinsia ya kiume sambamba na kulipa kipumbele suala la Upambanaji.
“Hatutarajii kuona mwanaume aliyehudhuria kongamano hili la Grumeti aweke hereni wala kusuka nywele, vaeni uhalisia wa kiume katika Upambanaji ili kujenga jamii bora” ukilipa kipaumbele suala la maadili kwani ndio msingi wa kila kitu katika maisha”. alisema Rwakatare.
Kwa takribani miaka saba kampuni ya Grumeti Fund imekuwa ikitoa elimu ya kijinsia kwa wanafunzi wa kike na kiume katika shule za sekondari mbalimbali Wilayani Serengeti na Bunda ambapo tangu mwaka 2017 hadi awamu ya kwanza ya kongamano hili kwa Mwaka 2024 imefanikiwa kutoa elimu ya kijinsia kwa wasichana 11,092 na kutoa taulo za kike kwa kila binti anayeshiriki mafunzo hayo, huku ikifanikiwa kutoa mafunzo kwa wavulana zaidi ya 3,995 tangu mwaka 2021 hadi awamu ya kwanza ya kongamano la Mwaka 2024 na kutoa zawadi za jezi na mipira kwa kila shule iliyoshiriki kwenye kongamano.